Miquissone hatari sana

Tuesday October 06 2020
miquissone pic

WINGA Luis Miquissone juzi alikuwa moto wa kuotea mbali kwa kutoa mchango mkubwa katika ushindi wa mabao 4-0 ambao Simba iliupata ugenini dhidi ya JKT Tanzania katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Mbali ya bao alilofunga na pasi moja ya mwisho aliyopiga, Miquissone aliwaweka katika wakati mgumu, viungo na walinzi wa JKT Tanzania kutokana na kasi, chenga na pasi zake ambazo zilifika eneo husika kwa usahihi mara kwa mara alipokuwa na mpira na hata pale ambapo hakuwa nao.

Kiwango cha nyota huyo kilipunguza kasi ya idadi kubwa ya wachezaji wa JKT Tanzania kupanda mbele kushambulia na kulazimika kujikita zaidi katika ulinzi jambo ambalo lilifanya lango la timu yake liwe salama kwa muda mrefu.

Ni mchezo ambao pamoja na Simba kuutawala kwa muda mrefu, walionekana kunufaika zaidi na makosa ya wachezaji wa safu ya ulinzi ya JKT Tanzania hasa wale wa kati ambao walionekana kukosa mawasiliano, kutojipanga katika nafasi sahihi pindi walipokuwa wakishambuliwa lakini pia ufanisi duni katika ukabaji.

Mbinu ya kutumia mipira ya juu ambayo Simba waliitumia na uwezo wa washambuliaji wao hasa wa kati, Chris Mugalu na Meddie Kagere ilionekana kuwapa shida JKT Tanzania na haikushangaza kuona wakiruhusu mabao matatu kwa staili inayofanana.

Iliwachukua Simba, dakika sita tu mara baada ya filimbi ya kuanza kwa mchezo kupulizwa kuandika bao la kwanza kupitia kwa Meddie Kagere aliyeunganisha kwa kichwa krosi ya Larry Bwalya na dakika mbili baadaye, Mugalu akaongeza la pili akimalizia kwa kichwa krosi ya Luis Miquissone.

Advertisement

Dakika nne kabla ya filimbi ya muda wa mapumziko kupulizwa, Kagere tena aliifungia Simba bao la tatu likiwa la pili kwa upande wake katika mchezo huo, akimalizia kwa shuti kali la mguu wa kushoto pasi ya Clatous Chama na dakika ya 54, Miquissone aligongelea msumari wa mwisho katika jeneza la JKT Tanzania baada ya kuifungia Simba bao la nne akimalizia kwa shuti kali la mguu wa kushoto mpira uliookolewa na walinzi.

 

 

Advertisement