Miquissone atwaa tuzo

KIUNGO wa pembeni wa Simba, Luis Miquissone amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Machi wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020/2021 huku Mohamed Badru wa Gwambina amechukua tuzo hiyo kwa kuwa kocha bora.

Miquissone na Badru walitwaa tuzo hizo, baada ya kuwashinda wenzao walioingia nao fainali kwa mwezi Machi katika uchambuzi uliofanywa wiki hii na kamati ya tuzo ya VPL, kutokana na mapendekezo ya makocha waliopo vituo mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa.

Kwa Machi, Miquissone alikuwa na mchango mkubwa kwa timu yake na kuonesha kiwangocha kuvitia, ambapo Simba ilishinda mchezo  mmoja na kutoka sare moja, huku mchezaji huyo akifunga mabao mwili na kuchangia asisti ya bao.

Wachezaji ambao waliingia nao kwenye  fainali  hizo ni Idd Seleman wa Azam FC na Paul Nonga wa Gwambina FC.

Kwa upande wa kocha Badru, alitwaa tuzo hiyo, baada ya kuiongoza Gwambina kushinda michezo miwili na kutoka sare mmoja na kupanda kutoka nafasi ya 15 hadi 11, timu yake ikiifunga Ihefu mabao 2-1,Mtibwa Sugar mabao 2-0 na kutoka suluhu na nyumbani na Tanzania Prisons.

Wachezaji ambao wametwaa tuzo tayari ni ya mwezi kwa msimu huu  Prince Dube wa Azam (Septembe),Tonombe Mukoko wa Yanga (Oktoba), John Bocco wa Simba (Novemba), Saido Ntibazonkiza wa Yanga (Desemba), Deogratius Mafie wa Biashara (Januari) na Anuary Jabir wa Dodoma Jiji (Februari).

Kwa upande wa makocha ambao walishatwaa tuzo hizo ni Aristica Cioba aliyekuwa Azam (Septemba), Cedrick Kaze aliyekuwa Yanga (Desemba), Charels Mkwasa wa Ruvu (Novemba), Kaze (Desemba), Francis Baraza kipindi yupo Biashara United (Januari) na Zuber Katwila wa Ihefu (Februari).

Kadhalika, Meneja wa uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Modestus Mwaluka ametwaa tuzo ya Meneja bora wa Uwanja kwa mwezi Machi, 2021.