Miquissone aitanguliza Simba mapema Kirumba

Muktasari:

Miquissone alifunga bao hilo dakika ya 27 kwa mpira wa faulo baada ya Kapombe kuangushwa nje kidogo ya eneo la hatari.

Mwanza. Makosa yaliyofanywa na Polisi Tanzania haswa kuonekana kupaniki na kujaa presha yameonekana kuinufaisha Simba na kuwafanya kwenda mapumziko kuwa mbele kwa bao 1-0.

Katika mchezo huo ambao unapigwa uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, ulionekana kuwa wa nguvu na hesabu kubwa kwa timu zote kusaka japo bao ili kujiweka pazuri kwenye vita ya pointi tatu.

Simba walionekana kulisakama zaidi lango la Polisi Tanzania tangu mapema, jambo lililowafanya mabeki wa Maafande hao kuonekana kupaniki kuzuia hatari zilizokuwa zikilenga lango lao.

Kutokana na presha hiyo iliwafanya kucheza rafu za mara kwa mara ambazo katika hali nyingine ziliwanufaisha wapinzani kwa kujipatia bao kupitia kwa Luis Miquissone dakika ya 27 kwa shuti lake la moja kwa moja nje ya uwanja.

Miquisone alifunga bao hilo kufuatia beki wa kulia, Shomari Kapombe kuangushwa nje kidogo ya eneo la hatari na kuweza kuwaamsha mashabiki kwa bao hilo.

Hata hivyo Polisi Tanzania walijaribu kutengeneza mashambulizi lakini walionekana kuzidiwa na Wekundu hao ambao walionesha soka safi na la mahesabu licha ya kwamba walishindwa kutumia vyema nafasi walizopata.

Mwamuzi, Ahmada Simba (Kagera) hakusita kuwatembezea kadi za njano wachezaji wa Polisi Tanzania, Abdulraziz Makame dakika ya 10 na Hassan Nassor dakika ya 39 kwa kumchezea Miquisone rafu kwa nyakati tofauti.