Mike Tyson aenda jela miaka sita kesi ya kubaka

Muktasari:
Siku ya pambano Tyson na Douglas waliingia ulingoni kila mmoja akiwa amevurugwa. Tyson changamoto za maisha na ujana, Douglas alikuwa ametoka kumpoteza mama yake mzazi siku 23 kabla ya pambano.
KATIKA sehemu iliyopita ya makala haya ya bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, Mike ‘Iron’ Tyson, tuliangalia jinsi mkwanja ulivyompa jeuri, akatimua makocha na kuoa. Endelea….
Baada ya kumpiga The Truth, nje ya ulingo Tyson aliendelea kuteswa na ujana. Misukosuko ikawa mingi. Matokeo yakaonekana Februari 11, 1990, baada ya kupigwa KO raundi ya 10 na Mmarekani mwenzake Buster Douglas.
Kuelekea pambano lenyewe, wacheza kamari na wachambuzi walimpigia upatu Tyson kwa zaidi ya asilimia 97. Hawakujua kuwa Tyson waliyemwamini siye huyo. Alishakuwa wa tofauti kabisa.
Siku ya pambano Tyson na Douglas waliingia ulingoni kila mmoja akiwa amevurugwa. Tyson changamoto za maisha na ujana, Douglas alikuwa ametoka kumpoteza mama yake mzazi siku 23 kabla ya pambano.
Pambano lilipoanza ndipo Tyson ambaye hakuwa wa kawaida alipoonekana. Alionekana kukosa ufundi na hakuwa akipigana kama bingwa. Raundi ya 10, Douglas alimfumua Tyson ‘uppercut’ kisha kumuongezea ‘jab’ nne za haraka, yaani ‘Four-Punch Combo’, Tyson akakaa ulingoni kwa mara yake ya kwanza katika historia yake ya ndondi.
Refa wa mchezo, Octavian Meyran, alimhesabia Tyson ambaye alishindwa kunyanyuka. Tukio hilo linatajwa kuwa la mshangao na mshtuko mkubwa zaidi katika ndondi. Bondia hatari, mwenye ngumi katili, aliyeogopwa, alikalishwa akiwa kijana mdogo wa miaka 23.
Mwaka huohuo (1990), Tyson alirejea ulingoni mara mbili dhidi ya Henry Tillman na Alex Stewart, yote mawili alishinda kwa KO raundi ya kwanza. Ushindi dhidi ya Tillman, ulimpunguzia machungu, kwani Tillman alimshinda mara mbili Tyson kwa pointi mwaka 1984, wakati wa ngumi za ridhaa, kisha kwenda Olimpiki na kutwaa medali ya dhahabu.
Bondia Evander Holyfield, alimpiga Douglas hivyo kutwaa ubingwa wa dunia, sasa Tyson akawa na kibarua cha kupigana na Evander ili kuutwaa ubingwa kwa mara nyingine, hasa baada ya kushinda mapambano yote ya mtoano dhidi ya Tillman, Stewart na Donovan Ruddock ‘Razor’ mara mbili.
Pambano likiwa limepangwa Novemba 8, 1991, Tyson aliumia mbavu mazoezini, hivyo mchezo ukafutwa.
Na baada ya hapo Tyson aliingia kwenye kesi ya kumbaka mrembo aliyeshinda taji la Miss Black American na kufungwa jela miaka sita.
Hata hivyo, Tyson alitumikia kifungo cha miaka mitatu na kuachiwa kwa msamaha. Kipindi akiwa jela, aliamua kubadili dini kuwa Muislam na kuchagua jina la Malik Abdul Aziz.
Kwa nini Tyson alifungwa? Jawabu ni ujana. Inaelezwa kuwa ushahidi haukuwepo wa kutosha na Tyson alieleza kuwa mrembo huyo ndiye ambaye alimtaka kimapenzi. Hata hivyo, majibu ya jeuri mahakamani kutokana na kiburi cha fedha na umaarufu, yalimtibua jaji, hivyo akamfunga ili akajifunze adabu.
TYSON AKARUDI
Alipotoka jela, Tyson alirejea vizuri ulingoni kwa kushinda mapambano mawili mfululizo, Peter McNeely na Buster Mathias Jr. Pambano dhidi ya McNeely liliingiza fedha nyingi sana kutokana na shauku kubwa ya mashabiki kumuona Tyson baada ya kumkosa kwa miaka minne.
Machi 1996 Tyson alimpiga Frank Bruno kwa mara ya pili kwa KO raundi ya tatu na kurejesha mkanda wa WBC, kisha akampiga Bruce Seldon na kubeba mkanda wa WBA. Alikuwa amerudi vizuri zaidi.
Kurejesha mikanda miwili kwa kushinda mapambano manne, mawili yasiyo ya ubingwa, vilevile mawili ya ubingwa, kulimfanya Tyson arejeshe kiburi, akawa yuleyule aliyeanguka kwa kupigwa na Douglas kisha kutupwa jela kwa ubakaji.
Novemba 9, 1996, Tyson akipewa nafasi kubwa dhidi ya Holyfield, alipokea kichapo cha TKO kwa kuokolewa na mwamuzi, Mitch Halpern raundi ya 11 baada ya kuona Tyson amezidiwa na hawezi kuendelea na mchezo. Waliporudiana Juni 28, 1997, pambano lilivunjika raundi ya tatu baada ya Tyson kumng’ata sikio Holyfield ambaye alipewa ushindi.
Pambano hilo la pili kati ya Tyson na Holyfield, liliweka rekodi nyingi, moja ni thamani yake ambayo ilidumu kwa miaka 10 katika ndondi kabla ya kuvunjwa mwaka 2007 na pambano kati ya Oscar De La Hoya dhidi Floyd Mayweather Jr. vilevile kuwa pambano la kwanza katika miaka 50 kuvunjika kutokana na mpinzani kutenguliwa ushindani.
Baada ya hapo Tyson alijitetea kuwa alimng’ata sikio Evander kwa sababu bondia huyo alimpiga kichwa na hakukatwa pointi. Alipoona uelekeo wa kufungiwa kupigana, Tyson alimuomba radhi Evander pamoja na jumuiya yote ya ndondi lakini hiyo haikuzuia kufungiwa.
Usikose mwendelezo wa makala haya kesho uone jamaa alivyojua kula bata na kitu kile alichowafanya madereva wawili walioigonga gari yake wakati akijiachia zake kitaani.