miezi sita ya Arajiga , Sasii

Muktasari:

  • Mwamuzi Ahamed Arajiga na Elly Sasii ni miongoni mwa waamuzi waliofungiwa na kamati ya waamuzi kwa zaidi ya miezi sita pamoja na waamuzi wengine waliondolewa kwenye ratiba na wengine kufungiwa miezi miwili hadi mitatu.

WAAMUZI wa kimataifa wa Tanzania ambao walifungiwa kutokana na makosa mbalimbali ya kujirudia kwenye michezo ya Ligi Kuu sasa wamerejeshwa na msimu ujao wataonekana wakiendelea na majukumu yao.

Mwamuzi Ahamed Arajiga na Elly Sasii ni miongoni mwa waamuzi waliofungiwa na kamati ya waamuzi kwa zaidi ya miezi sita pamoja na waamuzi wengine waliondolewa kwenye ratiba na wengine kufungiwa miezi miwili hadi mitatu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassoro Hamduni alisema baada ya tathmini juu ya waamuzi hao na wengine waliofungiwa sasa watarejea kazini kujiandaa na msimu ujao.

"Msimu ujao utaanza mapema hivyo hata sisi maandalizi yetu yataanza mapema kwani mwishoni mwa mwezi huu tutakutana na waamuzi wote wa Ligi Kuu na wale wa Ligi ya Championship ili kukumbushana kidogo.

"Ligi ikianza na tukagundua kuna waamuzi wana makosa yale yale ya kujirudia na walishafungiwa basi tutamwondoa kwenye orodha ya waamuzi ili akafanye kazi nyingine," alisema Hamduni.
Alisema msimu uliomalizika ulikuwa na mabadiliko makubwa kwao kwa kufanya kazi vizuri na kupunguza lawama kwa wadau ambao misimu kadhaa waamuzi ndio walikuwa wakitupiwa mzigo wa lawama kwenye michezo.

Aliongeza tayari mikoa imeanza kutoa mafunzo kwa waamuzi ngazi ya awali na wataendelea huku semina kwa waamuzi wa First League na ligi za chini wakiwa wanaandaliwa mafunzo yao kulingana na kalenda yao ambayo itatoka wiki hii.

Baadhi ya waamuzi waliofungiwa vifungo tofauti msimu uliomalizika hivi karibuni ni pamoja na Emmanuel Mwandembwa, Hussen Athuman, Nassor Mwinchui, Florentino Zablon, Elly Sasii, Arajiga, Amina Kyando na Rafael Ikambi.
Waamuzi wengine wa kati ni Jackson Palangyo, Hance Mabena, Hilbert Marine, Ahmed Simba wakati wa pembeni ni Mary Mwakitalama, Rashid Zongo, Hamis Chang'walu, Jesse Erasmo, Kassim Mapanga, Fredinand Chacha na Soud Lila.

Agosti 15 mwaka jana Bodi ya Ligi (TPLB) katika kikao kilichofanyika Arusha kilifanya maboresho ya kanuni mbalimbali ikiwemo ya kuthibiti waamuzi kwa kuwaonya, kuondolewa kwenye ratiba, kushushwa daraja na kuondolewa kwenye orodha ya waamuzi wanaotambulika na TFF.

Waaamuzi wa kati walioanza kuchezesha Ligi Kuu walikuwa 32 huku waamuzi wa pembeni walikuwa 42 kati ya hao 15 Waamuzi wenye kitambaa cha Fifa huku watano waamuzi jinsi ya kike ambapo yupo, Jonesia Rukyaa na Tatu Maloko (kati) waamuzi wa pembeni ni Janeth Balama, Glory Tesha na Zawadi Yusuph.

Wanaume wenye kitambaa cha Fifa ni Arajiga, Sasii, Ramadhan Kayoko, Siyah Saluni (kati) waamuzi wa pembeni ni Hashim Zawadi, Mohamed Mkono,  Sound Lila, Frank Komba,  Ally Ramadhan, Kassim Mpanga na Said Ally.