Mhilu: Nyota ya Kagera isiyoonekana Taifa Stars

Katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, wafungaji wameendelea kuwa wageni katika mbio za kuwania kiatu cha ufungaji bora.

Msimu uliopita, mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere aliibuka na tuzo hiyo baada ya kufikisha mabao 22, akiibuka na tuzo hio kwa msimu wa pili mfululizo na kujiwekea heshima katika ufungaji.

Wakati hali ikiwa hivyio kwa misimu miwili, bado tatizo la wazawa katika ufungaji limezidi kuwa kubwa kutokana na msimu huu pia kuanza kwa kusuasua.

Hadi sasa, washambuliaji wakongwe wa Tanzania wameshindwa kuonyesha makali yao kutokana na kuachwa na wageni.

Wakati Prince Dube akiongoza katika ufungaji hadi sasa kwenye michezo suita akiwa na mabao sita, anafuatiwa na raia wa Zambia, Obrey Chirwa, wote wa Azam FC.

Katika orodha hiyo ya mabao, pia yumo Kagere, ambaye ameanza vizuri utetezi wa tuzo yake licha ya kuanza msimu kwa shida mbele ya John Bocco mwenye bao moja pekee

Chris Mugalu raia wa Congo naye ana mabao matatu, sawa na Bigirimana Blaise wa Namungo raia wa Burundi na Meshack Abraham wa Gwambina.

Lakini katika orodha hiyo, yumo pia mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Yusuph Mhilu, ambaye ameonyesha kuwa Mtanzania hatari zaidi katika ushambuliaji kwa sasa.

Hatari ya Mhilu inatokana na kucheza mechi tatu na kufunga katika kila mchezo, hakuanza katika mechi za awali za ligi kutokana na kuwa majeruhi, lakini kurejea kwake kumekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha kocha Mecky Maxime.

Licha ya Kagera Sugar kutokuwa na mwenendo mzuri katika Ligi Kuu kwa sasa, Mhilu ameonyesja kuwa na uwezo tofauti kama Maxime atafanikiwa kupata dawa ya kuirejesha timu kwenye mstari.

Katika msimamo wa ufungaji, Dube wa Azam raia wa Zimbabwe ndiye anaongoza akiwa amefunga matano akifuatiwa na Mnyarwanda, Meddie Kagere wa Simba mwenye mabao 4.

Mhilu ambaye msimu uliokwisha alimaliza Ligi Kuu akiwa na mabao 13 nyuma ya Kagere aliyetwaa kiatu cha dhahabu ana ndoto ya kuwatoa kwenye reli wazawa katika vita ya ufungaji.

“Sijacheza mechi tatu tangu msimu kuanza dhidi ya JKT, Gwambina na Yanga nilikuwa mgonjwa, lakini ndoto yangu ya kiatu cha dhahabu msimu huu ipo pale pale,” anasisitiza Mhilu.

Maxime amzungumzia

Kocha wa mchezaji huyo, Mexime wa Kagera Sugar anasema katika mechi tatu ambazo Mhilu amecheza, amekuwa na wakati mzuri na kuwa injini ambayo inaleta matumaini kikosini.

Maxime anasema kama atafanikiwa kupata suluhisho la vipigo vyake, ni wazi kuwa Mhilu ataonyesha cheche zaidi na mabao yake kuonekana tofauti na sasa.

“Amefunga dhidi ya KMC, Azam FC na Namungo, ni mshambuliaji mzawa ambaye anapambana,” aanasema Mexime.

Maxime anasema licha ya kwamba katika soka mshambuliaji hawezi kufunga kila mechi, lakini kama Mhilu angecheza mechi zote sita, bila shaka angekuwa juu zaidi ya alipo sasa kwenye orodha ya wafungaji msimu huu.

Kibadeni amsifu

Akizungumzia mwenendo wa Mhilu na ‘ubutu’ wa washambuliaji wazawa kwenye ligi, kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema mshambuliaji kufunga ndiyo kazi yake.

“Ukimuona mshambuliaji anacheza mara kwa mara na hafungi, maana yake ni kwamba hajitumi au kiwango chake kina mashaka,” alisema.

Anasema washambuliaji wa kigeni wanaokuja kucheza nchini wanakuja kwa malengo, ndiyo sababu wanafanikiwa katika maelngo yao kwa kujitoa na kutaka kutimiza alichokipanga.

“Kwa Mhilu anajitahidi, anapambana, lakini kinachowasumbua washambuliaji wetu wazawa ni kutocheza kwa malengo,” anasema kocha huyo na mchezaji wa zamani wa Simba, Kibaden.

Anasema Mhilu, ambaye alijiunga Kagera akitokea Ndanda aliyokua anacheza kwa mkopo kutoka Yanga SC ambako alikuwa akicheza kama winga ni zaidi ya wachezaji waliokuja wa kimataifa nchini kama atapewa nafasi ya kuonekana mara kwa mara uwanjani.

“Unaweza usimuone kwa sasa, lakini ni moja ya wachezaji wazuri pengine kuliko hata hawa wa kimataifa ambao tunawaona katika timu za Ligi Kuu,” anasema.