Mgunda: No Chama, No problem

Muktasari:

  • Mgunda na msadizi wake, Seleman Matola wana kibarua kizito mbele yao ambacho ni kuhakikisha chama hilo linamaliza msimu likiwa katika nafasi mbili za juu ili kupata tiketi ya msimu ujao kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

WAKATI mabadiliko ya kikosi cha Simba katika michezo miwili iliyopita ya ligi yakianza kuwavutia baadhi ya wadau na mashabiki wa timu hiyo, kaimu kocha mkuu wa wekundu hao wa Msimbazi, Juma Mgunda anaamini wanaweza kufanya makubwa zaidi katika michezo saba iliyosalia kabla ya msimu 2023/24 kumalizika bila ya uwepo wa baadhi ya mastaa akiwemo Clatous Chama anayesumbuliwa na majeraha lakini pia amefungiwa mechi tatu.

Mgunda na msadizi wake, Seleman Matola wana kibarua kizito mbele yao ambacho ni kuhakikisha chama hilo linamaliza msimu likiwa katika nafasi mbili za juu ili kupata tiketi ya msimu ujao kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kocha huyo ambaye hii ni awamu yake ya pili kukaimu nafasi hiyo Simba, alisema miongoni mwa mambo ambayo ameyafanyia kazi mbali na mbinu ni kuwajenga wachezaji kisaikolojia kwa kuwa bado wana nafasi ya kufanya kitu katika michezo iliyosalia.

“Haiwezi kuisha wakati bado, itaisha mpaka itakapoisha, tuna michezo mbele yetu hivyo hatuwezi kukata tamaa, tunatakiwa kufanya vizuri katika kila mchezo halafu baada ya hapo ndio tutaona wapi ambao juhudi zetu zitakuwa zimetufikisha,” alisema kocha huyo na kuongeza;

“Nina furaha na namna ambavyo vijana wanaonyesha kupokea maelekezo na wanavyoyafanyia kazi, kilichopo mbele ni kuendelea na mapemabano.”

Miongoni mwa wachezaji ambao wanaonekana kufanya vizuri wakiwa na Mgunda katika michezo miwili iliyopita ni pamoja na Saleh Karabaka na Edwin Balau ambao hapo kabla hawakuwa wakipata nafasi ya kucheza mara kwa mara chini ya Abdelhak Benchikha ambaye alibwaga manyanga baada ya kutwaa Kombe la Muungano.

“Wachezaji kama Edwin Balua na Ladaki Chasambi bado ni wadogo na uwepo wao hapa Simba maana yake wana uwezo mkubwa, kwangu najivunia na ni wakati wa kuwapa nafasi ya kucheza zaidi kwa sababu ya kasi waliyonayo pindi tunapotafuta matokeo chanya.

“Simba ina wachezaji wengi wazuri hivyo kila mmoja anaweza kutumika wakati wowote ule, ujue wale ambao wanakaa benchi sio kwamba uwezo wao ni mdogo, hapana, ni suala la nafasi tu kwa sababu wachezaji wanaoanza ni 11 tu.”

Mgunda aliongeza, katika michezo iliyobaki ataendelea kutoa nafasi kwa kila mmoja wao akiamini uwezo waliokuwa nao huku akiweka wazi ni sehemu ya vijana hao kukua zaidi kwa sababu wanapocheza mara kwa mara ndipo wanapozidi kujiamini.

“Ukiangalia mchezo wetu uliopita na Mtibwa Sugar kipindi cha kwanza kilipooza kidogo lakini baada ya kuwaingiza vijana kama Saleh Karabaka na wengine uliona kasi ya mechi iliongezeka hivyo kwangu najivunia sana uwepo wao hapa kikosini.”

Kwa upande wake, Balua aliyefunga bao moja katika mchezo dhidi ya Namungo ambao Simba ilitoka sare ya mabao 2-2, alisema; “Hakuna mchezaji ambaye anapenda kukaa benchi, niliamini wakati wangu utafika na nipata nafasi na pengine ndio huu, kiukweli nina njaa ya kuonyesha kuwa sikuja Simba kwa bahati mbaya.”

Mchezo unaofuata kwa Simba ni leo Jumatatu dhidi ya Tabora United ambayo inapambana kujinasua katika hatari ya kushuka daraja, huo utakuwa mchezo wa tatu kwa Mgunda tangu akabidhiwe mikoba akianza kwa kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Namungo, kisha akashinda 2-0 dhidi ya Mtibwa. Baada ya leo, Mei 9 Simba wataivaa Azam FC.

Ikumbukwe kuwa Azam ambayo ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 54 ndio wapinzani wakuu wa Simba wenye pointi 50 katika kinyang’aniro cha kumaliza msimu katika nafasi mbili za juu, wamepishana pointi nne huku Mnyama akiwa na mchezo mmoja nyuma.