Mgunda bado hajakata tamaa Simba

Muktasari:

  • Mgunda aliyerejesha furaha za Wanasimba kwa kupata matokeo mazuri tangu alipompokea Kocha Abdelhak Benchikha mwishoni mwa Aprili, amesema bado anaamini timu hiyo inaweza kumaliza nafasi ya pili na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

LICHA ya mashabiki wa Simba kuikatia tamaa timu hiyo kumaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na kuinasa tiketi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Azam FC iliyoganda nafasi hiyo kwa muda mrefu, kwa upande wa kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda hajakata tamaa kabisa.

Mgunda aliyerejesha furaha za Wanasimba kwa kupata matokeo mazuri tangu alipompokea Kocha Abdelhak Benchikha mwishoni mwa Aprili, amesema bado anaamini timu hiyo inaweza kumaliza nafasi ya pili na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 66 kama ilizonazo Azam, ila inazidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa, ikizidiwa manane na Wanalambalamba na keshokutwa Jumanne kila moja itakuwa uwanjani kumalizia msimu kwa kucheza mechi dhidi ya JKT Tanzania na Geita Gold zilizopo pabaya.

Azam itakuwa ugenini dhidi ya Geita iliyopo nafasi ya 15 katika msimamo ikiwa na pointi 25, huku Simba itakuwa nyumbani jijini Arusha kuikaribisha JKT Tanzania inayokamata nafasi ya 12 yenye alama 32 na zinapambana kuepuka kushuka daraja au kuangukia kwenye play-off ya kuepuka kwenda Championship.

Katika mechi 29 ilizocheza Simba, imeshinda 20 kutoka sare sita na kupoteza tatu ikifunga mabao 57 na kufungwa 25, wakati Azam nayo imecheza mechi kama hizo na kushinda pia 20, sare sita na kulala mara tatu ila imekwambisha wavuni mabao 61 na yenye kuruhusu nyavu zao kuguswa mara 21 tu.

Ili Simba imalize nafasi ya pili na kuipiku Azam ni lazima ishinde mechi dhidi ya JKT, huku Azam ipoteze au kutoka sare na Geita, vinginevyo ijiandae tu kuungana na Coastal Union kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, michuano iliyofika robo fainali misimu miwili iliyopita ilipotolewa Ligi ya Mabingwa.

Hata hivyo, Mgunda amesema bado anaamini wana nafasi licha ya kuonekana mlima mrefu kwa maana ya toafuti ya mabao manane kati yao na Azam.

"Katika mpira lolote linaweza kutokea kikubwa ni kusubiri hadi mchezo wa mwisho ila naamini tunaweza kumaliza nafasi ya pili," alisema Mgunda aliyewahi kung'ara na Coastal Union kama mchezaji akiwa mmoja wa wachezaji walitwaa ubingwa wa Ligi ya Bara mwaka 1988 na kushiriki michuano ya CAF mwaka 1989.

Mgunda pia amewahi kuinoa Coastal kama kocha mkuu kabla ya kunyakuliwa na Simba mara ilipoachana na Zoran Maki, enzi za uchezaji wake alikuwa ni straika na alisifika kwa kuwa na mashuti makali na aliisaidia Wagosi kufika fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame) 1989 iliyocheza Kenya na kupoteza kwa mabao 3-0 mbele ya Kenya Breweriers (sasa Tusker FC).

Kocha huyo amesema, licha ya Ligi kuendelea kuwa ngumu kutokana na mpinzani  uliopo na idadi hiyo ya mabao lakini kama mwalimu kazi yake ni kuandaa timu ili kufanya vizuri katika kila mchezo uliopo mbele yao.