Mgunda aanza mipango mapema

Muktasari:
- Namungo itakuwa mgeni wa Yanga, huku ikiwa na rekodi ya kutoshinda mbele ya vinara hao wa Ligi Kuu, na Mgunda amesema watashuka uwanjani na mikakati ya kipekee ili kufikia lengo la kuibakisha timu katika mashindano hayo.
KOCHA mkuu wa Namungo, Juma Mgunda ameipiga mkwara Yanga watakayokutana nayo Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam akisema ameanza kusuka mipango kuhakikisha wanapata ushindi kwa mara ya kwanza dhidi ya wenyeji wao katika Ligi Kuu Bara.
Namungo itakuwa mgeni wa Yanga, huku ikiwa na rekodi ya kutoshinda mbele ya vinara hao wa Ligi Kuu, na Mgunda amesema watashuka uwanjani na mikakati ya kipekee ili kufikia lengo la kuibakisha timu katika mashindano hayo.
“Mashabiki wa Namungo na viongozi kwa ujumla wanataka kuona tunashinda mechi dhidi ya Yanga. Nalifahamu hilo na naandaa mkakati mzuri wa kuhakikisha tunashinda. Hatutacheza kwa mazoea mchezo huo, na tunaendelea kuandaa timu ambayo itaingia uwanjani kishujaa na kushinda mechi,” alisema Mgunda.
“Hakuna mechi rahisi hasa mzunguko huu wa lalasalama kila timu imejiandaa kupambania nafasi kuna ambao wanautafuta ubingwa, wengine tano bora halafu kuna sisi ambao tunatafuta uhakika wa kucheza msimu ujao. Tunakutana na timu ambayo imekamilika kila idara na ipo kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji, mchezo hautakuwa rahisi.”
Mgunda alisema anaelewa ubora na ushindani watakaokutana nao, lakini hawaogopi kwa vile wanakiamini kikosi walicho nacho kuwa ni bora na chenye kupambana uwanjani.
“Makosa tuliyoyafanya kwenye uwanja wetu wa nyumbani tukikubali kupoteza kwa mabao 2-0 hatutayarudia na kama wao walishinda ugenini nasi tunaweza kufanya hivyo ugenini. Kikubwa ni kuwa na mipango thabiti itakayotutengenezea mazingira mazuri ya kubaki kwa msimu ujao.”
Namungo ipo nafasi ya tisa ikicheza mechi 27 ikikusanya pointi 31, ikishinda nane, sare saba na vipigo 12, huku rekodi zikionyesha katika mechi 11 zilizokutana Ligi Kuu tangu 2020, Yanga imeshinda sita na tano kuisha sare na hata kwenye ya Kombe la FA Yanga pia iliibuka mbabe.