Messi awafungisha tela mabeki Getafe
Muktasari:
Kwa Messi na Ronaldo kufunga mabao ni kama utaratibu wao wa kawaida, ingawa ni kweli kuwa si mabao yote yanapatikana kwa namna moja, na katika mabao yote waliyofunga kwa miaka kadhaa, kuna yanayoonekana kuwa ya viwango vya juu kuliko mengine.
KATIKA toleo lililopita mwandishi Luca Caioli alichambua rekodi za mabao za Ronaldo na kumalizia na Messi na baada ya hapo akagusia mabao ya kukumbukwa au matamu au ukipenda mabao ya kideo ya mastaa hao. Sasa endelea…
Kwa Messi na Ronaldo kufunga mabao ni kama utaratibu wao wa kawaida, ingawa ni kweli kuwa si mabao yote yanapatikana kwa namna moja, na katika mabao yote waliyofunga kwa miaka kadhaa, kuna yanayoonekana kuwa ya viwango vya juu kuliko mengine.
Kuna mabao ambayo yamekuwa muhimu na yenye kuamua matokeo, kuna mabao ambayo ni ya kuvutia, na kuna ambayo yanabaki kuwa alama ya mafanikio. Yafuatayo ni mabao sita ya kukumbukwa ya mastaa hao.
Messi: Barca vs Getafe
Ilikuwa mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme iliyopigwa Aprili 18, 2007. “Miaka 20, miezi 10 na siku 26 baadaye Messi anarudia bao la Maradon,” kilisomeka kichwa cha habari katika ukusara wa mbele wa gazeti la Marca ambalo ni gazeti maarufu la michezo la Madrid.
Asubuhi ya siku iliyofuata baada ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme mwaka 2007, vyombo vya habari vilikuwa na vichwa tofauti tofuati vya habari, chambuzi pamoja na lugha mbalimbali za kimichezo za aina tofauti tofauti kama vile Messidona na The foot of God na Messi shocks the world.
Na hili ndilo tukio ambalo vyombo vya habari vililizungumzia; ilikuwa katika dimba la Nou Camp, dakika ya 28, Messi anaambaa na mpira kutoka mbali wa kama mita 65 kutoka lango la yake na kuelekea timu pinzani.
Kwa kasi na chenga za maudhi, Messi aliwafungisha tela wachezaji wa Getafe, anawazidi ujanja mabeki wanne wa timu hiyo pamoja na kipa wao kisha anafumua shuti kwa mguu wa kulia, si kawaida yake na mpira kujaa wavuni.
Kwa kila aliyeshuhudia, bao hilo liliibua kauli za bao la karne, ambalo Diego Maradona alilifunga dhidi ya England katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1986 nchini Mexico.
Mashabiki wapatao 53,599 waliokua Nou Camp ni kama vile walikuwa miguuni kwa Messi, waliinua juu kila kitu kilichoweza kuinuliwa na kupunga mkono kuanzia leso, magazeti, skafu, au kingine chochote kilichowezekana.
Na kwa wale ambao hawakuwa na kitu chochote cha kukiinua walichofanya ni kutumia mikono yao kumpigia makofi Messi kwa kipindi kirefu hadi mikono kuuma. Heshima ya nguvu na ya kipekee kwa Messi.
Katika mtandao wa YouTube, bao hilo liliibua mjadala wa aina yake, ni bao ambalo liliangalia mara nyingi, maelfu, na kuibua mjadala kwenye mitandao ambako mashabiki wao kwa wao walikuwa wakiulizana kwamba bao lipi ni bora.
Kila mmoja alikuwa na mawazo yake, kutoka kwa wataalam wa soka na wale wenye kuongozwa na ushabiki wakati vyombo vya habari vilifanyia ulinganifu video hiyo katika kila ‘engo’ huku wakimpongeza Messi.
“Je Messi alikuwa akijaribu kumuiga Maradona? Au hilo ni tukio tu ambalo limejitokeza tu na hakuwa amepanga kulifanya? “Labda ni uchezaji ule ule, nimewahi kuona uchezaji huu kwenye televisheni mara moja tu,’’ alisema Messi.
“Hata hivyo sikuwahi kuwaza kama lingeweza kuwa kama lile bao la Diego (Maradona) waliniambia baadaye lakini wakati ule sikuwa nikifikiria chochote, kwangu ilikuwa ni furaha tu ya kufunga goli.”
Itaendelea Jumamosi ijayo