Meneja, Ngassa wamfungukia Mayele

ALIYEKUWA meneja wa mshambuliaji wa Pyramids, Fiston Mayele, Nestor Mutuale amemjibu kimtindo straika huyo akiipongeza klabu yake ya zamani ya Yanga kwa kuendelea kuwa na akili kubwa mbele ya mchezaji huyo.

Nestor ambaye ndiye aliyesimamia uhamisho wa Mayele kwa mara ya kwanza wakati anatua Yanga amesema Mayele ameonyesha kutokuwa muungwana kwa klabu hiyo kwa kushindwa kuheshimu mambo mazuri ambayo klabu hiyo ilimfanyia wakati alipokuwa hapa Tanzania.

Nestor ameipongeza Yanga kwa kuwa kimya bila kumjibu mshambuliaji huyo akisema hilo ni jibu kubwa ambalo litamuhukumu Mkongomani mwenzake huyo kwa kuichafua klabu ambayo ilimtengenezea jina kubwa.

"Nani alikuwa anamjua Fiston (Mayele) kabla? Alipofika Yanga mambo yalikuwaje? Unawezaje kusema vibaya juu ya nyumba ambayo imekutengenezea rekodi kubwa, hakuna mabaya ambayo yanaweza kufifisha mazuri ambayo mdogo wangu Fiston aliyapata Yanga," amesema Mutuale.

"Nawapongeza Yanga wameonyesha ni klabu inayoongozwa na viongozi wenye akili kubwa kwa kuamua kunyamaza, hata mimi wameniambia nisiseme kitu lakini hapana acha niongee kidogo kwa kuwapongeza, ukimya wao ni jibu kubwa kwenda kwa Fiston, hata mashabiki wa Yanga waige akili ya viongozi wao, ule upendo waliomuonyesha utajibu mambo ambayo anawafanyia sasa."


MSIKIE NGASSA

Staa wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa naye amemjibu Mayele kupitia ukurasa wa Instagram akisema mshambuliaji huyo kama ana tatizo lolote na mtu ndani ya klabu hiyo atafute namna ya kumalizana naye.

"Ila swahiba wangu mfungaji bora wewe kweli wa kusema, mimi najua... lakini mimi ninachojua nyota yako ipo Yanga, karibu Tanzania," ameandika Ngassa huku akiongeza;

"Kama kuna tofauti zozote na viongozi malizana nao mjomba, wewe ni mfungaji bora, katika dunia hii mimi ni shabiki yako namba moja, piga kazi ndugu yangu kama kuna mtu kakukosea malizana naye sio Yanga, utapata dhambi, kuna watu wanakufa kwa sababu yako wanavyokupenda na kuona unayosema, Tanzania ni familia yako mjomba hata mimi ni shabiki yako sana, kila jema mjomba."

Kauli za meneja wa zamani wa Mayele na nyota huyo wa kimataifa anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi katika timu ya taifa hadi sasa, imekuja baada ya straika huyo wa Pyramids kukaririwa mara kadhaa akiishutumu Yanga kumfanya ashindwe kucheza vyema kwa sasa akiwa Misri.

Pia amekuwa akitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kulumbana na wanayanga na juzi kati akifanyiwa mahojiano ya kituo cha Azam TV na alitoa shutuma nzito zilizosababisha mahojiano hayo yaondolewe mtandaoni kwa kilichodaiwa Yanga iliandika barua kulalamikia kile kilichorushwa hewani dhidi yao.

Hadi anaondoka Yanga, Mayele ndiye aliyekuwa mfungaji kinara wa klabu hiyo kwa misimu yote miwili aliyoichezea akitokea AS Vita, akifunga mabao 16 msimu wa kwanza na kumaliza na 17 kama Mfungaji Bora msimu uliopita sambamba na Saido Ntibazonkiza wa Simba, huku akiwa pia Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho Afrika ambalo Yanga ilicheza fainali kwa mara ya kwanza na kupoteza mbele ya USM Alger Algeria iliyobeba taji kwa kanuni ya faida ya mabao ya ugenini kwani matokeo yalikuwa 2-2.

Yanga ilifungwa nyumbani mabao 2-1, bao la kufutia machozi la timu hiyo ikiwekwa kimiani na Mayele likiwa ni la saba kwake katika michuano hiyo, kisha ikaenda kushinda ugenini 1-0 kwa bao la penalti la Djuma Shaban ambaye hayupo kwa sasa kikosini na Waalgeria kubeba ndoo kwa kanuni hiyo ya CAF.