Mechi inayofuata baada ya kipigo kikubwa -2

Muktasari:

  • Mchezo wa Aprili 20 utakuwa wa kwanza baina ya jamaa hawa tangu Novemba 5, 2023 ambapo Yanga iliiadhibu vikali Simba kwa mabao 5-1

TUNAENDELEA na mfululizo wa makala zetu za kuelekea mechi ya watani wa jadi, Aprili 20, 2024.

Mchezo wa Aprili 20 utakuwa wa kwanza baina ya jamaa hawa tangu Novemba 5, 2023 ambapo Yanga iliiadhibu vikali Simba kwa mabao 5-1.

Katika sehemu ya kwanza tuliona utata wa mchezo uliofuata baada ya kipigo kikubwa cha 5-0 ambacho Yanga walikitoa kwa Simba, Juni Mosi, 1968.

Leo tutakuletea simulizi ya mechi iliyofuata baada ya kipigo kikubwa cha 6-0 ambacho Simba waliwapa Yanga, Julai 19, 1977. Endelea.

Kipigo cha 6-0 cha 1977 ndicho kikubwa zaidi katika vipigo vyote ambavyo hutokea baina ya wababe hao wa soka nchini.
Baada ya kipigo hicho mechi ya kwanza baina yao ilitakiwa ifanyike mwaka 1978 lakini haikufanyika kwa sababu Yanga walijitoa kwenye ligi baada ya mechi mbili tu za kwanza yaani ligi ikiwa bado mbichi kabisa.


Navy Zanzibar 0-0 Yanga
Pamba Shinyanga 2-0 Yanga
Yanga ılıjitoa kabla hata tarehe ya mechi yao dhidi ya watani wao haijapangwa, kwa madai kwamba kulikuwa na njama za waamuzi kuwakwamisha.

Viongozi wa Yanga walisema walijitoa ili kuepusha uvunjifu wa amani kwani mashabiki wao wasingeweza kuvumilia kuona timu yao inaonewa na waamuzi, kwamba lazima wangefanya fujo.
Sasa ili kuepuka fujo hizo, ndipo Yanga wakaamua kujitoa kwenye ligi ikiwa inaendelea.

Katika mechi hizo mbili za kwanza, Yanga ilipata kipigo cha nyumbani cha mabao 2-0 kutoka kwa Pamba ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) katika mechi iliyofanyika Machi 8, 1978.

Kipigo hicho kilikuwa kichungu sana kwa Yanga ambayo bado ilikuwa ikijitafuta tangu ifukuze nyota wake kadhaa mwaka 1976.
Hadi wakati huo, msimamo ulikuwa kama ifuatavyo.

 NB: Navy Zanzibar kwa sasa ndiyo KMKM. Wakati huo ushindi ni alama mbili, siyo tatu kama sasa.

Baada ya Yanga kujitoa, Chama cha Soka Tanzania (FAT) kikabariki uamuzi huo na kuzipa ushindi wa mabao mawili na alama mbili timu zote zilizotakiwa kucheza na Yanga.

Pia Yanga ikafungiwa kwa muda wa miezi mitano kuanzia Julai hadi Desemba.

Navy Zanzibar wakaibuka na vitisho wakitishia kujitoa kwenye ligi wakipinga uamuzi wa FAT kugawa pointi za Yanga kama njugu.

Lakini baadaye yakafanyika mazungumzo ya kikubwa na wakakubali kuendelea na ligi.
Kwa hiyo mechi ya kwanza baada ya kipigo kikubwa ambayo ilipaswa kufanyika mwaka 1978 haikufanyika.
Yaani msimu wa kwanza ukapita kavu bila wakongwe hawa kukutana.

Baada ya msimu wa 1978 kupita kavu kavu wakaja kukutana msimu uliofuata wa 1979, na hii ndiyo simulizi yake.
Mchezo huo ulifanyika Oktoba 7, 1979 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru), na Simba kushinda mabao 3-1.

Wafungaji wa mabao ya Simba walikuwa Nico Njohole ‘OCD’ dakika ya tatu. Hili lilikuwa moja ya mabao bora kwani mfungaji alichukua ‘kijiji’ kabla ya kufunga.
Mohamed Bakari ‘Tall’ dakika ya 38 na Abbas Dilunga dakika ya 72.

Bao la kufutia machozi la Yanga lilifungwa na Rashid Hanzuruni dakika ya nne.

Yanga wakawa wamepigwa tena na Simba na kushindwa kulipa kisasi.

Simba
Athuman Mambosasa
Daud Salum “Bruce Lee”
Mohamed Kajole
Filbert Rubibira
Mohamed Bakari “Tall”
Abbas Kuka
George “Best” Kulagwa
Nico Njohole
Adam Sabu
Abdallah Mwinyimkuu
Abdallah Hussein/Abbas Dilunga

Yanga
Bernard Madale
Rajab Tangale
Hussein Kondo “Mmakonde”
Charles Boniface Mkwassa
Suleiman Jongo
Rashid Idd
Ayub Shaaban
Juma Mkambi
Rashid Hanzuruni
Omar Hussein “Keegan”
Ahmed Omari
Kwa faida tu ya wasomaji wetu, huu ndiyo mwaka ambao Simba walifanya majaabu Afrika kwenye mashindano ya klabu bingwa.
Walifungwa nyumbani mabao 4-0 na Mufurira Wanderers ya Zambia na kwenda kupindua meza ugenini kwa kushinda 5-0.
Ni kikosi hicho ndicho Yanga walitakiwa kukilipizia kisasi. Ilikuwa vigumu.
Mchezo huo utakumbukwa zaidi kama mchezo wa kwanza baina ya watani wa jadi kushuhudia ndugu wawili wa familia moja wakichezea timu mbili tofauti.
Simba walikuwa na Abdallah Hussein na Yanga walikuwa na Omari Hussein.
Mchezo huu ulionyesha wazi kwamba Yanga wana safari ndefu kujenga timu baada ya kuwafukuza wale nyota wao wengi mwaka 1976.