Mchezaji mwingine afariki dunia uwanjani

Muktasari:

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Songwe (Sorefa), Jacob Mwangosi amesema ni masikitiko makubwa kumpoteza mchezaji huyo ambaye alishiriki Ligi ya Mkoa.

VIFO vya wachezaji kufariki uwanjani vimeendelea kuleta simanzi nchini, baada ya mchezaji mwingine kupoteza maisha wakati wa mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwinga wilayani Mbozi mkoani Songwe.

Hii ni mara ya pili ndani ya miaka miwili kupoteza wachezaji uwanjani, baada ya Aprili 10 mwaka jana, mchezaji Albert Andrea aliyekuwa akiichezea Saza FC kufariki alipogongana na mwenzake wakiwania mpira.

Jana Jumatano simanzi nyingine ilitawala wakati wa mechi ya kirafiki baina ya Manchester FC na Super Eagles kwa mchezaji, Bille Mgala kuanguka wakati akiwania mpira na kupoteza maisha.

Kocha wa Manchester FC na ndugu wa marehemu huyo, Onivi Mgala amesema tukio hilo lilitokea katika dakika 33 ambapo mchezaji huyo alikuwa akirukia mpira wa juu na mpinzani wake aliyemkingia mgongo na kudondoka na kupoteza fahamu.

“Ulipigwa mpira wa juu sasa ile anaruka, beki wa Super Eagle akamkingia mgongo ndio akadondoka na kupoteza fahamu, tulipompeleka kituo cha Afya Isense wakasema tumpeleke Mbozi Mission ambako alikuwa amekata roho,” amesema Mgala.

Mgala amesema marehemu huyo hakuwa na matatizo yoyote kiafya na alikuwa mchezaji mwenye uwezo na kipaji haswa kwenye eneo la ushambuliaji akiwa tegemeo kikosini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani Songwe (Sorefa), Jacob Mwangosi amesema ni masikitiko makubwa kumpoteza mchezaji huyo ambaye alishiriki Ligi ya Mkoa.

“Changamoto kubwa pia ni mazingira ya miundombinu, pia wachezaji na hizi timu hawana tabia ya kupima afya haswa magonjwa ya moyo, kwetu ni masikitiko makubwa,” amesema Mwangosi.

Baadhi ya matukio yaliyowahi kutokea nchini kwa wachezaji wakiwa uwanjani ni lile la Hussein Tindwa aliyekuwa Simba aliyeanguka uwanjani kwenye mechi ya Caf, mwaka 1979 dhidi ya Racca Rovers ya Nigeria, pia kipa wa AFC Arusha, Nadhiri Mchomba mwaka 2001 katika mechi dhidi ya 44 KJ ya Mbeya.

Wengine waliofariki uwanjani ni chipukizi wa Coastal Union U20, Mshauri Salim aliyeanguka 2015 mjini Tanga, pia kuna Ismail Khalfan wa Mbao U20 aliyeanguka katika ligi ya vijana mwaka 2016 mjini Kaitaba timu ya Mbao ilipokuwa ikiumana na Mwadui na Januari mwaka juzi mchezaji wa timu ya vijana wa Singida FG, Mohammed Banda naye alifariki uwanjani wakati wa mazoezi ya timu mjini Singida.