Mcameroon wa Prisons ana mtihani mzito

PAMOJA na kufanya vizuri kwenye mazoezi ya timu, lakini straika wa Tanzania Prisons, Roland Messi, raia wa Cameroon ameendelea kusugua benchi ilhali tangu atue kocha Ahmad Ally hajaonja dakika yoyote ya mchezo wa Ligi Kuu.

Nyota huyo mwenye mwili wake, alisajiliwa mapema msimu huu chini ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Fredi Felix 'Minziro' lakini licha ya matarajio ya wengi, staa huyo hakuweza kuonyesha makeke hadi kutupwa benchi.

Hata hivyo, katika kipindi cha Minziro, Mcameroon huyo alikuwa akitokea benchi huku mchezo mmoja pekee dhidi ya Tabora United akianza na kuishia dakika 45 kisha akapumzishwa, ambapo tangu Ally atue hajagusa uwanjani tena.

Pia straika huyo alikuwa katika orodha ya waliokuwa watemwe dirisha dogo licha ya uongozi kushindwa kutekeleza hilo kutokana na masuala ya madai ya mishahara aliyokuwa anaidai timu na kipengele cha kuvunja mkataba.

Messi alitua nchini kujaribu bahati yake tangu msimu uliopita,  ambapo alianzia African Sports ya Tanga ambako hakufanikiwa kabla ya kuibukia kwa Wajelajela ambao waliona vitu vyake uwanjani na kumpa kandarasi ya mwaka mmoja.

Nyota huyo ameiambia Mwanaspoti kuwa licha ya kutokuwa na namba, lakini bado anaendelea kupambana haswa mazoezini kulishawishi benchi la ufundi kumuamini ili kuendeleza kipaji chake akieleza kuwa matarajio ni kupata namba.

Amekiri vita kuwa ngumu kikosini kutokana na wenzake kuonyesha ushindani na hali hiyo inampa changamoto kuongeza juhudi na akili binafsi ili kuweza kupenya katika kikosi hicho.

"Ushindani ni mkali na kila mmoja anapambania namba, bado sijakata tamaa na lolote linaweza kutokea, ligi haijaisha kimsingi ni kuzidi kujituma mazoezini na kuongeza juhudi binafsi," amesema.