Mbrazili amaliza bifu la Mwenda, Kapombe
Muktasari:
- Awali inaelezwa mabeki hao walikuwa hawaivi, kiasi cha Mwenda kudaiwa kugoma kujiunga na timu licha ya kupona majeraha yake, japo mabosi wa klabu hiyo walikuwa wakificha, ila habari za ndani zinasema kazi kubwa iliyofanywa na Mbrazili kumaliza bifu hilo.
BENCHI la ufundi Simba chini ya Kocha Oliveira Robertinho limekata mzizi wa fitina kwa kumaliza bifu linalodaiwa kuwapo baina ya mabeki wa kulia, Shomary Kapombe na Israel Mwenda baada ya kuwaweka chini na sasa kila kitu kinaenda sawa.
Mabeki hao ni kati ya wachezaji waliopo kwenye safari ya kikosi cha Simba kilichopo Guinea kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AC Horoya.
Awali inaelezwa mabeki hao walikuwa hawaivi, kiasi cha Mwenda kudaiwa kugoma kujiunga na timu licha ya kupona majeraha yake, japo mabosi wa klabu hiyo walikuwa wakificha, ila habari za ndani zinasema kazi kubwa iliyofanywa na Mbrazili kumaliza bifu hilo.
“Robertinho na jopo lake waliwaweka chini na kurekebisha mambo na kila kitu sasa kipo sawa ndio maana umeona Mwenda kajiunga na timu na ameungana na wenzake kwenye msafara baada ya kukosekana kwa muda mrefu,” kilisema chanzo makini kutoka ndani ya Simba.
Wakati huo huo urejeo wa mshambuliaji wake, Moses Phiri aliyekuwa kwenye kiwango bora kulingana na mazoezi yaliyofanyika ndani ya timu hiyo, kumezidi kuinogesha kambi ya Simba.
Simba kabla ya kwenda Guinea, Phiri alikuwa kwenye kiwango bora na kuonyesha dalili ya kutaka kucheza mechi ya Horoya kwani alifunga mabao mawili makali.
Phiri anaweza kuchukua nafasi ya Saido Ntibazonkiza (ambaye ni majeruhi) dhidi ya Horoya kama hataanza ataingia kipindi cha pili utakuwa mchezo wake wa kwanza kucheza wa kimashindano tangu alivyoumia katika dhidi ya Kagera Sugar.
Rekodi zinaonyesha Phiri aliyefunga mabao 10 kwenye ligi ni miongoni mwa wachezaji hatari katika kikosi cha Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwani kwenye hatua za awali amefunga mabao matano. Kikosi cha Simba kimewaacha nyumbani wachezaji wengine wanne nchini, Ntibazonkiza, Jonas Mkude, Jimmyson Mwanuke na Peter Banda.
Ratiba ya simba CAF
Horoya vs Simba -Feb 11
Simba vs Raja CA -Feb 18
Vipers vs Simba -Feb 25
Simba vs Vipers-Machi 7
Simba vs Horoya -Machi 18
Raja CA vs Simba -Machi 31