Mbrazil wa Singida BS hadi msimu ujao

Muktasari:

  • Dario aliyejiunga na Singida Big Stars mwanzoni mwa msimu huu na kuanza kwa makali na kuwa kivutio kwa mashabiki nchini lakini akaandamwa na majeraha ambapo Januari 27, 2023 klabu yake ilimpa ruhusa ya kwenda kwao Brazil kupata matibabu.

HAMU ya mashabiki wa soka nchini na wapenzi wa Singida Big Stars kumuona winga wa timu hiyo, Dario Frederico raia wa Brazil akicheza uwanjani katika mechi zilizobaki za Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (ASFC) msimu huu imeyeyuka baada ya klabu hiyo kueleza kuwa nyota hajawa fiti kwa asilimia 100.

Dario aliyejiunga na Singida Big Stars mwanzoni mwa msimu huu na kuanza kwa makali na kuwa kivutio kwa mashabiki nchini lakini akaandamwa na majeraha ambapo Januari 27, 2023 klabu yake ilimpa ruhusa ya kwenda kwao Brazil kupata matibabu.

Akieleza maendeleo ya mchezaji huyo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo Ijumaa, Afisa Habari wa klabu hiyo, Hussein Massanza amesema nyota huyo amemaliza likizo yake ya siku 30 (mwezi mmoja) na ripoti ya daktari inaonesha amepona kwa zaidi ya asilimia 90.

Amesema licha ya kuwa fiti kwa sasa, mchezaji huyo ataungana na kikosi cha Walima Alzeti hao wakati wa maandalizi ya Ligi Kuu msimu ujao wa 2023-2024.

“Mchezaji wetu Dario Frederico amemaliza likizo yake ya mwezi mmoja na ripoti ya daktari inaonesha amepona kwa zaidi ya asilimia 90, hata hivyo, klabu kupitia kwa ushauri wa kitaalamu wa daktari imemuongezea muda Dario aweze kuwa timamu kwa asilimia 100 apate na muda wa kutosha wa kupumzika,”

“Kutokana na maamuzi haya, mchezaji wetu huyu Fundi raia wa Brazil ataungana na kikosi rasmi wakati wa maandalizi ya ligi kuu msimu ujao, wadau na mashabiki wetu watarajie kumuona akiwa kwenye kiwango bora zaidi atakapoungana na timu kwenye kambi yetu ya Pre-season nchini Tunisia,” amesema Massanza.