Mbona Ulimwengu kazi anayo Sudan

BAADA ya kuambulia pointi moja kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Thomas Ulimwengu na wenzake watakuwa na kibarua kizito huko Sudan kupigania pointi tatu za kwanza katika hatua ya makundi dhidi ya Al-Hilal Omdurman.

Ulimwengu na mastaa wenzake wa TP Mazembe walichemka katika mchezo wa kwanza ambao ulipigwa Lubumbashi na kuambulia pointi hiyo moja huku wenzao, Al-Hilal Omdurman. wao wakikiona chamoto Afrika Kusini, walichezea kichapo cha mabao 2-0.

Kipigo cha Al-Hilal Omdurman kutoka kwa Mamelodi Sundowns na sare ambayo waliipata Mazembe vinaufanya mchezo huo kutegemewa kuwa na ushindani wa aina yake.

Katika mchezo huo, ambao utachezwa keshokutwa Jumatano, Februari 24 atashuhudiwa Ulimwengu akirejea nyumbani, Omdurman kutokana na miaka ya nyuma kuichezea miamba hiyo ya soka la Sudan kabla ya kupata dili la kujiunga na JS Soura ya Algeria.

Bila shaka kocha wa TP Mazembe, Pamphile Mihayo Kazembe anaweza kumtumia Ulimwengu mwenye mabao matatu kwenye mashindano hayo kama silaha yake muhimu kwenye kikosi cha kwanza kutokana na mshambuliaji huyo kuifahamu vizuri Al-Hilal Omdurman.

Licha ya Ulimwengu kuifahamu vizuri Al-Hilal Omdurman anatarajiwa kukutana na upinzani mkali kutoka kwa Faris Abdalla ambaye amekuwa akifanya vizuri na timu.

Baada ya mchezo huo, TP Mazembe watarejea kwao DR Congo kwa ajili ya maandalizi ya kuivaa Mamelodi Sundowns katika mechi yao ya tatu itakayopigwa Machi 5.