Mbombo, Akaminko kikaangoni Azam

Muktasari:

  • Habari ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo anataka kupitisha panga kwenye kikosi chake na kuwa na wachezaji ambao anaamini ataenda nao vizuri akiwa anaifundisha timu hiyo.

Mastaa wa Azam FC, Idris Mbombo, James Akaminko na Abdulai Iddrisu wamekalia kuti kavu na huenda wakatolewa kwa mkopo katika dirisha dogo msimu huu linalotarajia kufunguliwa Disemba 16 mwaka huu.

Habari ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo anataka kupitisha panga kwenye kikosi chake na kuwa na wachezaji ambao anaamini ataenda nao vizuri akiwa anaifundisha timu hiyo.

Katika hilo ni wazi Dabo alianza kuwaondoa polepole mastaa wake kwenye kikosi cha kwanza huku akiwa hajawajumuisha Akaminko na Iddrisu katika kikosi chake kilichocheza mechi za ugenini dhidi ya Mashujaa na Ihefu.

Mechi hizo zote ambazo mastaa hao wamekosekana Azam imeshinda, ilishinda 3-0 dhidi ya Mashujaa na 3-1 dhidi ya Ihefu hali ambayo inazidi kuchochea hali ya wachezaji hao kutemwa.

Inadaiwa kuna sintofahamu kati ya Dabo na mastaa hao baada ya kutofurahia kiwango ambacho wamekionyesha kwenye mechi za nyuma.

Alipotafutwa Ofisa habari wa Azam FC, Thabit Zakaria 'Zaka' kuzungumzia mastaa hao kukosekana kama ni wagonjwa alisema wamekosekana kwa sababu za kiufundi.

"Hao wachezaji wamekosekana kwa sababu za kiufundi, hata wao wakati wanacheza kuna wengine walikuwa hawachezi;"

"Amoah yeye alikosekana kwa sababu aliumia kwenye maandalizi ya mechi (Warm Up) mechi na Ihefu tukiwa kule ugenini."