Mbili zapanda Ligi Kuu Zenji, Zimamoto yaua

Muktasari:
- Muembe Makumbi ilikata tiketi ya kucheza Ligi Kuu kwa msimu ujao baada ya juzi kuifumua New King kwa mabao 2-0 katika mechi ya play-off iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung, mjini Unguja siku moja tu baada ya Inter Zanzibar kutangulia kwa kuinyoosha Paje Stars kwa mabao 2-1 pia kwenye uwanja huo huo.
WAKATI maafande wa KVZ na Zimamoto wakifanya mauaji katika mechi za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) iliyopo ukingoni, timu za Muembe Makumbi na Inter Zanzibar zimekuwa za kwanza kupanda ligi hiyo kwa msimu ujao wa 2024-2025.
Muembe Makumbi ilikata tiketi ya kucheza Ligi Kuu kwa msimu ujao baada ya juzi kuifumua New King kwa mabao 2-0 katika mechi ya play-off iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung, mjini Unguja siku moja tu baada ya Inter Zanzibar kutangulia kwa kuinyoosha Paje Stars kwa mabao 2-1 pia kwenye uwanja huo huo.
Timu hizo ni kati ya nne zinazopaswa kupanda Ligi Kuu kwa msimu ujao kuchukua nafasi ya timu zitakazoshuka kutoka kwenye ligi hiyo ambapo hadi sasa Maendeleo na Jamhuri zote za Pemba zikiwa zimeshaaga mapema, licha ya kusaliwa na michezo kadhaa ya kufungia msimu wa 2023-2024.
Maendeleo inayoburuza mkia ni kati ya timu zilizocheza ligi hiyo kwa mara ya kwanza msimu huu, lakini imeshindwa kuhimili vishindo kwa kuburuza mkia kwa muda mrefu, huku ikigeuzwa jamvi la wageni kwa kufumuliwa idadi kubwa ya mabao katika mechi inazochezea kwa siku za karibuni.
Moja ya mechi iliyogawa takrima ni ya jana jioni ilipofungwa mabao 4-1 na Zimamoto katika mechi iliyopigwa Uwanja wa FFU Finya, Pemba na kuwafanya wageni kurejea nafasi ya pili nyuma ya JKU kwa kufikisha pointi 56 baada ya mechi 25.
Katika mechi hiyo mabao ya Zimamoto yaliwekwa kimiani na Haruna Jabir dakika ya 25, Rashid Salum (dk 73), Amour Hussein (78) na Seif Khamis (81), huku bao la kufutia machozi la Maendeleo likiwekwa wavuni na Salim Abdallah dakika ya 90.
Kipigo hicho kilikuwa ni cha 21 kwa timu hiyo, huku ikiruhusu nyavu zao kuguswa mara 68 na kufunga 25 tu katika mechi 28 na kusaliwa na pointi 15 hadi sasa, nne pungufu na ilizonazo Jamhuri iliyopo nafasi ya 15 ikiwa nayo imeshashuka kulingana na kanuni za ZPL inayoshusha timu nne za mwisho kila msimu.
Katika mechi nyingine iliyopigwa pia jana kwenye Uwanja wa Mao B, mjini Unguja KVZ ilitakata kwa kuinyoa New City kwa mabao 3-0, ambapo Halifa Hassan Nolo alifunga mara mbili dakika ya 32 na 85 huku Sabri Dahari Omar akipigilia msumari wa mwisho dakika ya 81.
Ushindi huo umeifanya KVZ kufikisha pointi 50 baada ya mechi 27, huku New City ikisalia nafasi ya 10 ikiwa na pointi 33 baada ya mechi 28.