Mbeya Uwsa Queens yakaa mguu sawa

Muktasari:
- Timu hiyo inayomilikiwa na Mamlaka ya Maji jijini Mbeya, inajiandaa kushiriki ligi hiyo itakayofanyika jijini Arusha kuanzia Agosti 1, ikiwa ni mara ya kwanza kwao kucheza mashindano hayo.
WAKATI Mbeya Uwsa Queens ikiendelea na mazoezi kujiandaa na Ligi Kuu ya Netiboli, benchi la ufundi na mastaa wa timu hiyo wameonekana kupania wakitamba kufanya kweli na kuandika rekodi katika michuano hiyo.
Timu hiyo inayomilikiwa na Mamlaka ya Maji jijini Mbeya, inajiandaa kushiriki ligi hiyo itakayofanyika jijini Arusha kuanzia Agosti 1, ikiwa ni mara ya kwanza kwao kucheza mashindano hayo.
Hata hivyo, wababe hao wamekuwa na matokeo mazuri katika michuano kadhaa, ambapo kwa mara ya kwanza wakicheza ligi daraja la pili huko Katavi, walimaliza nafasi ya tatu, huku katika mashindano ya kikanda wakibeba ubingwa mkoano Iringa.
Meneja wa timu hiyo, Meshack Nyuha alisema licha ya kuwa mara yao ya kwanza kucheza ligi hiyo, wanaamini wataonesha ushindani na kutwaa ubingwa kutokana na maandalizi waliyonayo.
Alisema tangu walipojihakikishia kupanda daraja, timu imekuwa kambini kwa muda wote, huku wakifanya usajili kulingana na mahitaji ya timu, akieleza kuwa kiu yao ni kutwaa ubingwa.
“Hatuogopi yeyote, tumejipanga nje na ndani kuhakikisha ligi hiyo tunaandika rekodi na historia, tunajua wapo wazoefu ila kwa kikosi tulichonacho hatuoni wa kutusumbua” alitamba Meneja huyo.
Nahodha wa kikosi hicho, Coletha Fungo alisema kwa muda waliokaa kambini wamekuwa na muunganiko bora hivyo wanasubiri muda ufike waingie uwanjani kuonesha uwezo wao.
“Tumekuwa na muda wa kutosha kujiandaa kwa mechi kadhaa, imetupa muunganiko na kusaidia kujua udhaifu wetu, kimsingi tunaomba sapoti ya wadau na tutawakilisha vyema” alisema Coletha.