Mbeya City yashikilia mkataba wa Sabilo

Muktasari:

  • Sabilo alisajiliwa na Mbeya City kutoka Namungo kwa mkataba wa miaka miwili lakini ameitumikia timu hiyo msimu mmoja na timu kushuka daraja na msimu ujao itashiriki Ligi ya Championship.

WINGA wa Mbeya City, Sixtus Sabilo amesema licha ya kupata ofa ya nane kutoka timu za Ligi Kuu lakini hawezi kwenda bila kupata baraka za uongozi wa Mbeya City.

Sabilo alisajiliwa na Mbeya City kutoka Namungo kwa mkataba wa miaka miwili lakini ameitumikia timu hiyo msimu mmoja na timu kushuka daraja na msimu ujao itashiriki Ligi ya Championship.

Nyota huyo aliyemaliza msimu na mabao tisa alisema katika uchezaji wake soka hajawahi kucheza timu ikashuka daraja hivyo msimu huu ndio umekuwa wa kwanza kwake.

"Hakuna kitu kibaya kama kushuka daraja haya maumivu ndio naona sasa namna wenzangu huko nyuma wakishuka nilikuwa nawashuhudia lakini sikuwahi kujua maumivu yake.

"Hii ni historia mbaya kwangu kwenye soka sababu moja ya malengo ni kuona timu ikifanya vyema hivyo kushuka daraja kwa Mbeya City hata yale malengo yangu nikisema yametimia haina maana yoyote," alisema Sabilo.

Kuhusu kusalia ndani ya kikosi hicho msimu ujao alisema ni mapema kwasababu tayari kuna ofa ya timu nane lakini anasubiri kupata baraka za uongozi wa Mbeya City.

"Soka ndio kazi yangu lakini sijazungumza biashara na timu yeyote sababu ya maumivu niliyokuwa nayo moyoni kuhusu Mbeya City lakini kuanzia wiki ijayo (wiki hii) nitajua wapi nitakuwepo msimu ujao."

Sabilo hakuweza kuweka wazi juu ya dili lake la kutakiwa na Geita Gold pamoja na JKT Tanzania japo alieleza kati ya timu nane zilizotuma ofa nazo ni miongoni, hata hivyo hakuna kiongozi wa Mbeya City aliyekuwa tayari kuelezea hilo.

Aliongeza msimu ulimalizika ulikuwa na ushindani mkubwa kuanzia mwanzo wa msimu lakini kwao ilikuwa bahati mbaya kupata matokeo mabaya tena mzunguko wa pili wa ligi.

Timu nyingine alizowahi kuzitumikia nyota huyo mbali ya Mbeya City na Namungo ni Polisi Tanzania, Stand United na KMC FC ndizo timu za Ligi Kuu alizozitumikia.