Mbeya City yaamka, yailima New Fighter

Tuesday September 14 2021
mbeya pic
By Saddam Sadick

Kyela. Baada ya kuangukia pua mechi iliyopita, leo Mbeya City wamefanya kweli kwa kuilaza New Fighter mabao 2-1 na kufufua matumaini ya kufuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano maalumu ya kujiandaa na msimu ujao.

Mbeya City ambayo inajiandaa na Ligi Kuu msimu ujao, ilianza vibaya kwa kipondo dhidi ya Mbeya Kwanza, ambapo leo ilikuwa ikipambana na wapinzani hao wanaojiandaa na Ligi ya Wilaya ya Kyela.

Hata hivyo nao New Fighter walikuwa wakipambana kusaka ushindi ili kujiweka pazuri, lakini licha ya kucheza na Nahodha wao, Gaudence Mwaikimba walijikuta wakilala tena ikiwa ni kipigo cha pili mfululizo baada ya awali kudundwa na Small Boys bao 1-0.

Katika mpambano wa leo, Mbeya City ikicheza na kikosi chake kamili, walionekana kuhitahi ushindi na kuweza kuibuka na mabao hayo yaliyowekwa wavuni na  Helbert Lukindo dakika ya 11 na Paul Nonga dakika ya 70.

Kwa upande wa New Fighter ambayo licha ya uchanga wao lakini waliweza kupata bao la kujifariji likifungwa na Nahodha wao, Mwaikimba dakika ya 89 na kuwaamsha mashabiki ambao wengi waliishangilia timu hiyo.


Advertisement
Advertisement