Mbao ya Stam yaikamia JKT Tanzania

Muktasari:

  • Mbao inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi saba, watakuwa wenyeji wa JKT Tanzania mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kirumba Mwanza Septemba 15, baada ya hapo itawakaribisha Simba na Prisons.

Mwanza. Baada ya kuvuna pointi saba ugenini kocha wa Mbao FC, Amri Said ‘Stam’ amesema kwa sasa nguvu zote ni katika mechi za nyumbani akianza na JKT Tanzania kuhakikisha hapotezi kitu.

Mbao inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi saba, watakuwa wenyeji wa JKT Tanzania mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Kirumba Mwanza Septemba 15, baada ya hapo itawakaribisha Simba na Prisons.

Kocha Said alisema wanaendelea kujiwinda vikali kuhakikisha wanavuna pointi 10 kabla ya kuwavaa bingwa mtetezi Simba, Septemba 20 mwaka huu.

Alisema ili kuhakikisha wanatimiza malengo hayo tangu Ligi imesimama kupisha michuano ya kimataifa kwa timu ya Taifa, Mbao haijalala na inaendelea kujifua ikiwamo kucheza mechi za kirafiki.

“Mipango yetu kwanza ni kushinda mechi ijayo dhidi ya JKT Tanzani ili tufikishe alama 10 kabla ya kuwavaa sasa Simba, ambapo tutakuwa na nguvu zaidi na morari, tunaendelea kujiandaa vyema,”alisema beki huyo wa zamani wa Simba.

Said aliongeza kuwa maandalizi yao yanalenga kupambana na mechi zote bila kujali ugenini wala ukubwa wa timu, hivyo kila mpambano kwao wanauona kama fainali.

Stam alisema kikubwa anahitaji Mbao kuondokana na changamoto ya kusubiri matokeo ya kujinasua na janga la kushuka daraja dakika za mwisho, hivyo mashabiki wazidi kuisapoti timu yao.