Mayele ampiga bao Kramo wa Simba mchezaji bora Afrika

Muktasari:
- Mayele aliyeipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika anaongoza mbio hizo huku akiwapiga chini mastaa wanane
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Fiston Mayele anaongoza kwa kura kwenye mbio za mchezaji bora wa ndani wa Afrika kwa mwaka huu katika kiny'anganyiro hicho kinaendelea kupitia mtandao wa Foot Afrika.
Mayele aliyeipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kuifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika anaongoza mbio hizo huku akiwapiga chini mastaa wanane.
Katika upigaji huo wa kura unaoendelea Mayele ambaye ndiye mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho akiwa na mabao saba anaongoza kwa 40.04% akifuatiwa na Mahmoud Kahraba wa Al Ahly mwenye 34.45%.
Khaled Bousseliou wa USM Alger na timu ya taifa ya Algeria anashika nafasi ya tatu kwa kupata 8.00%, Percy Tau wa Al Ahly anashika ya nne na 6.23% huku Bouly Sambou wa Wydad Casablanca akiwa na 2.90%.
Nyota mpya wa Simba, Aubin Kramo aliyetokea ASEC Mimosas anashika nafasi ya sita akiwa na 2.90%, Hamza Khabba wa Raja Casablanca ana 1.99% wakati Souaibou Marou wa Coton Sport akiwa na 1.94%.
Peter Shalulile anayeichezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini anashika nafasi ya tisa akiwa na 1.56%.
Mayele pia ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 17 sawa na nyota wa Simba Mrundi, Saidi Ntibazonkiza 'Saido'.