Maxime aahidi balaa Kagera Sugar

MBEYA. POINTI nne walizovuna jijini hapa zimempagawisha Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime huku akiwapongeza vijana wake kwa kazi waliyoifanya huku akiahidi kuendeleza moto mechi zilizobaki.

Kagera Sugar katika mechi mbili ilizocheza kwenye Uwanja wa Sokoine ilishinda mechi moja dhidi ya Prisons bao 1-0 na sare ya mabao 2-2 mbele ya Mbeya City na kupanda nafasi ya tisa kwa pointi 15.

Kwa sasa timu hiyo itakuwa nyumbani kucheza mechi tano mfululizo ikianza dhidi ya Mtibwa Sugar, Novemba 28, kisha Ihefu Desemba 2, Azam, Geita Gold kisha Simba kabla ya kutoka kuwafuata Singida Big Stars, Januari 31 mwakani.

Maxime alisema haikuwa kazi nyepesi kuondoka na pointi nne, japokuwa hesabu na mipango yao ilikuwa ni kushinda mechi zote na vijana wake walifanya kazi nzuri.

Alisema pamoja na ugumu ulivyo kwenye ligi kwa timu kuonyesha upinzani, lakini Kagera Sugar kwa soka inaloonyesha itafanya vizuri akibainisha mechi zinazofuata hawataki kuacha kitu.

“Niwapongeze zaidi vijana wangu, wanaonyesha ari na morari kuipambania timu, haikuwa kazi ndogo kwa sababu Mbeya City na Prisons ni timu nzuri ila huu ni mwanzo tunaenda kuwasha moto zaidi,” alitamba Maxime aliyerejea hivi karibuni kikosini.

Kiungo wa timu hiyo, Abdalah Seseme alisema katika misimu mitatu nyuma hawakuwa na matokeo mazuri, hivyo hawataki kurudia makosa akisema wanahitaji ushindi kila mchezo bila kujali nyumbani au ugenini.