Maxi, Ngoma wapewa Dabi

Muktasari:

  • Simba ni mwenyeji wa mchezo huo wa raundi ya nane, wote wakiwa na pointi 18 lakini wakipishana mchezo mmoja ambao Simba imecheza mechi sita na Yanga saba ikiwa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

DABI ya Kariakoo inapigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam, Jumapili kuanzia saa 11:00. Mastaa wa zamani wenye uzoefu na mchezo huo wamesema eneo la kiungo likiongozwa na Maxi Nzengeli na Fabrice Ngoma litaamua mchezo.

Simba ni mwenyeji wa mchezo huo wa raundi ya nane, wote wakiwa na pointi 18 lakini wakipishana mchezo mmoja ambao Simba imecheza mechi sita na Yanga saba ikiwa kileleni kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kumbuka Simba ina viungo Mzamiru Yassin, Clatous Chama, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Saido Ntibazonkiza, Luis Misquissone na Kibu Denis.

Huku Yanga wakiwa na Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Jonas Mkude, Zawad Mauya, Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Maxi Nzegeli, Jesus Moloko na Farid Mussa ambao baadhi wanatakiwa kucheza mchezo huo.

Kenny Mwaisabula ambaye ni mchezaji wa zamani wa Bandari ya Mtwara,alisema mchezo huo utakuwa na ushindani mkubwa na itakuwa dabi nzuri na kali kuwahi kutokea kutokana na vikosi vya pande zote mbili kuwa imara.

“Mechi hiyo Yanga wa viungo wakali sana na wa kuchungwa muda wote japokuwa Simba na wao wanao wazuri ila wanapishana katika vitu vidogo ambavyo ni muhimu sana.

“Simba viungo wao wanatakiwa kuwa makini zaidi maana viungo wa Yanga wako vizuri, wanatakiwa kufanya kazi kubwa ya ziada kuhakikisha wanawadhibiti akina Pacome, Mudathir, Aziz KI, Maxi na wengineo,”alisema Mwaisabula ambaye ni Kocha wa zamani wa Yanga.

Beki wa zamani wa Simba, Said Sued ‘Panucci’ alisema mechi hiyo itatawaliwa na bato kali kwenye safu ya kiungo kwani kila timu ina viungo wazuri na kocha atakayechanga karata yake vizuri ataibuka na ushindi.

“Timu zote zina wachezaji wazuri kwenye eneo la kiungo, lakini wana utofauti kidogo, nikianza na Yanga wana viungo wao watatu ambao wametengeneza kombinesheni kali sana Aziz Ki, Maxi na Pacome na kitu ambacho naweza kusema timu hiyo imebahatika kwa sasa ni kwamba viungo wao wote ni wafungaji wazuri tofauti na Simba ambayo viungo wao wanafunga mara mojamoja.

“Viungo wa Simba licha ya kwamba siyo wafungaji wa mara kwa mara lakini wako vizuri sana katika kutuliza timu inapokuwa kwenye presha jambo ambalo linaweza kuwasaidia.Pia wana uwezo mkubwa wa kuanzisha mashambulizi,”alisema Sued ambaye alikuwa anajulikana kwa jina la Scud kutokana na uwezo mzuri wa kupiga mashuti.

Mrage Kabange ambaye ni winga wa zamani wa Simba, yeye aliunga mkono suala la viungo, lakini akawa tofauti kwa kusema kuwa anaamini Simba wanaweza kuwatumia watu wao wa katikati kutawala mchezo huo na kupata ushindi.

“Ukiangalia Simba inavyocheza sasa hivi hasa kwa viungo Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute ambaye naye amerejea kwa kasi unaona jinsi ganiwatakavyoweza kuibeba timu yao katika mchezo huo wakishirikiana na Mzamiru na Chama. Simba ni watulivu sana kwenye eneo lao la kiungo.

“Kwa upande wa Yanga kwa sasa wana viungo wazuri ambao wana uwezo mkubwa wa kufunga lakini wengi sio watulivu hali ambayo inaweza kuwapa nafasi kubwa Simba kutawala mchezo huo,” alisema Kabange ambaye wa zamani wa Kagera Sugar.

Amri Kiemba aliyekiwasha Simba, Yanga na Azam na sasa ni mchambuzi wa soka,alisema ingizo jipya la viungo wa Yanga limezidi kunogesha safu hiyo akiwemo Pacome na Maxi, lakini anaamini Ngoma atakuwa na siku nzuri sana.

Staa huyo aliyeibukia Kagera Sugar kabla ya kukipiga timu za Kariakoo, alisema Ngoma amekuwa msaada mkubwa ndani ya kikosi cha Simba kutokana na namna ambavyo ana uwezo mkubwa anaweza kuanzisha mashambulizi kuanzia nyuma na kukontro timu wakati huko nyuma alikuwa Kanoute na Mzamiru baada ya Jonas Mkude kuondoka.

“Kuongezeka kwa Ngoma Simba kumeleta uhai mkubwa, Yanga wana utajiri mkubwa eneo la katikati Simba wao pembeni wako vizuri hivyo basi mipango ya makocha itaamua pia japokuwa kiungo ndiyo sehemu ambayo inaonyesha uhai wa timu husika.

“Siwezi kusema nani atakuwa bora kuzidi mwenzake kwa kuwa kuna wachezaji wazuri kama Chama ambao michezo mingine wanafanya vizuri ikija kwenye dabi unashangaa kiwango chake ni kawaida, ikitokea akina Maxi, Pacome wakawa vilevile tulivyowazoea kiungo Yanga itakuwa bora kuliko Simba,”alisema Kiemba ambaye alikuwa na misimamo mikali ya kimasilahi enzi za uchezaji wake.

Nani ataamua huu mchezo, tupe utabiri wako; 0658-376 417