Matumaini Simba yatoweka, Azam, yanga 2-1

Wachezaji wa Yanga wakishangilia wakati walipokabidhiwa kombe lao
Muktasari:
Yanga ilishuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa tayari na ubingwa huku Simba ikiombea mabingwa hao wapate ushindi dhidi ya Azam ili ifufue matumaini yao ya kuipata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwani ilikuwa vitani kuwania nafasi ya pili.
MASHABIKI wa Simba walikuwa wakiipigia goti Yanga na kuiambia; Shemeji tusaidie, lakini Yanga wamewapuuza na kuwanyima nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani baada ya jana Jumatano kufungwa mabao 2-1 na Azam katika pambano la kiporo la Ligi Kuu Bara.
Yanga ilishuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa tayari na ubingwa huku Simba ikiombea mabingwa hao wapate ushindi dhidi ya Azam ili ifufue matumaini yao ya kuipata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwani ilikuwa vitani kuwania nafasi ya pili.
Hata hivyo kilichotokea katika pambano hilo lililojaa vituko baada ya uwanja kugeuka bwawa la kufugia samaki kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kuanzia jana mchana, ni Yanga kukubali kichapo hicho na kutibua sherehe zao za kukabidhiwa kikombe katika matokeo yaliyoidia Azam kunyakua tiketi ya Kombe la Shirikisho kwa kuiwakilisha Tanzania kimataifa kwa mara ya nne mfululizo.
Yanga ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kupitia kwa Mbrazili Andrey Coutinho, aliyefunga kwa mkwaju mkali wa adhabu ndogo baada ya Mrisho Ngassa kuchezwa madhambi. Bao hilo liliamsha shangwe kwa mashabiki wa Yanga na wa Simba waliokuwa wakiwashangilia katika mchezo huo.
Hata hivyo bao hilo halikudumu, kwani dakika mbili baadaye, Brayson Raphael aliisawazishia Azam kwa shuti kali akiunganisha krosi pasi ya Kpre Tchetche ambaye aliupiga mpira ambao Gaudence Mwaikimba aliukosa kuunganisha na Domayo kumaliza kazi.
Jambo la kustaajabisha ni kwamba bao hilo la Azam lilishangiliwa kwa pamoja kati ya mashabiki wa Azam, Yanga na baadhi ya mashabiki wa Simba kitu ambacho siyo cha kawaida kushuhudiwa kwenye uwanja huo.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko ya wachezaji, ila ni Azam walionufaika na mabadiliko hayo baada ya kujipatia bao la pili la la ushindi katika dakika ya 78 kupitia beki wake, Aggrey Morris aliyemalizia mpira mrefu wa Shomary Kapombe.
Kwa matokeo hayo ya ushindi, Azam imefikisha pointi 48 ambazo haziwezi kufikiwa na Simba hata kama wataifunga JKT Ruvu keshokutwa katika pambano la kufungia msimu, kwani Vijana hao wa Msimbazi wenye pointi 44 watafikisha pointi 47 tu ambazo haziwasaidii kitu.
YANGA: Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Pato Ngonyani/ Kelvin Yondani, Salum Telela/Edward Charles, Danny Mrwanda, Nizar Khalfan, Amissi Tambwe, Mrisho Ngassa na Andrey Coutinho.
AZAM: Mwadini Ali, Himid Mao, Gadiel Michael, Shomary Kapombe, Aggrey Morris, Mudathir Yahya, Bryson Raphael, Frank Domayo/ John Bocco, Gaudence Mwaikimba/ Didier Kavumbagu na Kipre Tchetche.
Katika hatua nyingine, Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Sepp Blatter, ametuma salamu za pongezi kwa klabu ya Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Bara.