Matola: Aletwe mzungu yeyote

Wednesday June 22 2022
matola pic
By Clezencia Tryphone

KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Seleman Matola, amesema yuko tayari kufanya kazi na kocha yeyote yule ambaye ataletwa kwa ajili ya kuinoa timu hiyo.

Simba iko kwenye mchakato wa kusaka kocha mkuu atakayeungana na Matola baada ya Pablo Franco kufungashiwa virago kutokana na mwenendo mbovu ulioshuhudiwa timu ikipoteza mataji makubwa yote mawili msimu huu.

Simba imepoteza taji lake la Ligi Kuu Bara ililodumu nalo kwa misimu minne mfululizo iliyopita na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ililolitwaa kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita.

“Huwezi kuchagua namtaka huyu simtaki huyu, utakuwa hujiamini na hujui unafanya nini, cha msingi ni kufanya kazi kwa manufaa ya timu yetu,” alisema Matola ambaye ni mchezaji wa zamani wa Simba na Supersport ya Afrika Kusini.

Kuhusu nani anakuja kufanya naye kazi, alisema hata yeye hafahamu anasubiri jambo likiwa tayari atajulishwa kwa kuwa yeye ndiye mwenyeji wake.

Matola amefanya kazi Simba akiwa msaidizi kwa makocha Patrick Ausseums, Seven Vandenbroeck, Didier Gomes pamoja na Pablo Franco hivyo ni kocha mzawa mwenye uzoefu mkubwa wa kufanya kazi na wazungu.

Advertisement

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya Simba zinaeleza kwamba kocha raia wa Slovakia, Jozef Vukusic ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kutua Msimbazi. Simba inakamilisha ratiba ya Ligi Kuu Bara na imeanza usajili mpya kwaajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa.

Advertisement