Mastraika Taifa Stars wanahitaji maombi

Muktasari:

  • Mara ya mwisho kwa Samatta kufumania nyavu ilikuwa Novemba 12, mwaka jana alipoifungia PAOK bao katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Paneitolikos.

Wakati zikibaki siku 44 kabla ya mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Zambia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, mwenendo wa wachezaji wa safu ya ushambuliaji ambao wamekuwa wakitegemewa na timu ya taifa ‘Taifa Stars’ umeanza kuleta hofu.

Idadi kubwa ya wachezaji hao wameonyesha kupoteza makali ya kufumania nyavu katika klabu zao jambo ambalo linaweza kuigharimu Stars siku za usoni ikiwa hakutakuwa na mabadiliko katika muda mfupi uliobaki kabla ya kuwa na jukumu la kuhakikisha Taifa Stars inavuna pointi tatu zitakazoiweka katika nafasi nzuri kwenye kundi E la mashindano hayo. Nahodha na mshambuliaji kiongozi wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayechezea PAOK ya Ugiriki amekuwa na ukame muda mrefu kufumania nyavu ambapo hadi leo ametimiza siku 169 bila bao katika mashindano kwenye klabu na timu ya taifa.

Mara ya mwisho kwa Samatta kufumania nyavu ilikuwa Novemba 12, mwaka jana alipoifungia PAOK bao katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Paneitolikos.

Mshambuliaji Kibu Denis wa Simba kuanzia Novemba 5, 2023 alipofunga dhidi ya Yanga hadi sasa, amefunga bao moja katika siku 192 alilolipata katika mchezo wa mwisho wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Kelvin John anayeitumikia KRC Genk ya Ubelgiji ndani ya siku 187 amefunga bao moja ambalo alilipata katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki wa Tanzania dhidi ya Mongolia ambapo kabla ya hapo, kwenye klabu yake alifunga Oktoba 23, mwaka jana.

Nyota wa Tanzania anayecheza Al Najmah ya Saudi Arabia, Saimon Msuva msimu huu amefunga mabao manne ambayo matatu ameifungia klabu huku moja akipachika katika timu ya taifa ilipokuwa inashiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).

Straika wa Yanga, Clement Mzize angalau ndiye ameonyesha uhai kati ya wanaopata nafasi Stars ambapo ameshapachika mabao matano kwenye Ligi Kuu.

Wakati mambo yakionekana kuwa magumu kwa washambuliaji ambao wamekuwa wakipata nafasi ya kuitwa Stars, wanaaonekana kufanya vyema kwa sasa ni wale ambao hawaitwi.

Mmojawapo ni Waziri Junior wa KMC ambaye hadi sasa anaongoza kwa kufumania nyavu akiwa amefunga mabao tisa kwenye Ligi Kuu na anashika nafasi ya tatu kwenye chati ya kufumania nyavu na mshambuliaji mzawa anayefuatia ni Samson Mbangula wa Tanzania Prisons aliyepachika mabao manane hadi sasa kwenye Ligi Kuu.

Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Juma Mgunda alisema wana imani kubwa washambuliaji hao watarudisha makali ya kufumania nyavu na wataendelea kuwa msaada kwa timu ya taifa.

“Muda ukifika hayo yote yatazungumzika kwa vile sasa tupo katika mchakato wa kuangalia nani ambaye atajumuishwa, lakini kimsingi tuna imani watafanya vizuri na tutateua wale ambao watakuwa na mchango mkubwa kwenye timu,” alisema Mgunda.

Mshambuliaji wa zamani wa Taifa Stars, Uhuru Selemani alisema wachezaji hao wanapaswa kuonyesha utofauti kwa vile ni tegemeo la taifa. “Mchezaji ambaye unavaa jezi ya timu ya taifa unatakiwa kuwa mfano kwa wengine, hivyo hiyo inapaswa iwe kengele ya ukumbusho kwa ndugu zangu kwamba mwelekeo sio mzuri na wanapaswa kuongeza bidii.