Mastaa Yanga wanataka ndoo

VITA haijaisha. Kama ulikuwa unadhani vita ya ubingwa kwa Simba na Yanga imeisha msimu huu, pole yako kwao mastaa wa Jangwani, wamesisitiza lazima wabebe ndoo msimu huu hata kama mipango yao ya Ligi Kuu Bara imeshayeyuka kwao.

Mastaa hao wa Yanga wamesema bado wana nafasi ya kubeba ubingwa wa pili msimu huu baada ya lile la kwanza la Kombe la Mapinduzi 2021 kwa kuweka nguvu katika michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) wakijiandaa kwa sasa kuvaana na Biashara United kwenye nusu fainali.

Kiungo fundi wa Yanga, Haruna Niyonzima alisema wachezaji wamejipanga kutolikosa taji la ASFC baada ya kuona katika Ligi Kuu, watani wao Simba wana faida ya michezo mingi mkononi hivyo kuamini wana nafasi kubwa ya kutetea ubingwa tena.

“Tunaangalia zaidi ASFC kwani hilo lipo wazi, juhudi ya timu ndio itafanya mafanikio yaonekane. Hakuna mchezaji asiyependa mataji ama medali ndio maana tunajipanga kuhakikisha tunalichukua taji la ASFC ili tukate tiketi ya CAF kwa jasho letu,” alisema Niyonzima.

Naye beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ alisema, licha ya Biashara kuwa na soka la ushindani, lakini wanajipanga iwe mvua ama jua kupigania ushindi.

“Maana ya ushindani nikupata kitu kizuri mbele ya ugumu. Tunajua ni mechi ya jasho, ila tutapambana kadri tuwezavyo ili kuingia fainali kisha kuchukua taji hili ambalo ni muda sasa hatujalibeba,” alisema beki huyo wa kati aliyekiri kwenye Ligi Kuu Bara ni miujiza tu iwatokee. kwa jinsi watani wao walivyo.