Mastaa Yanga wamtikisa Kaze

YANGA bado wapo kileleni mwa msimamo na kuwafanya mashabiki wao kuendelea kuwa na nyuso za bashasha hasa baada ya juzi usiku kupata ushindi mbele ya Mtibwa Sugar, lakini kasi ndogo ya mastaa wa timu hiyo hasa wa safu ya ushambuliaji imemshtua Kocha mkuu wao, Cedric Kaze.

Ipo hivi. Rekodi moja ya mastraika wake wawili, Michael Sarpong na Ditram Nchimbi imemtikisa Kocha Kaze ambaye ameapa kula nao sahani moja kuhakikisha wanarejea kwenye kiwango chao cha kutupia mabao kwenye mechi za Ligi Kuu Bara na zile za michuano mingine.

Kama hujui ni kwamba mara ya mwisho kwa Sarpong kufunga ilikuwa ni Novemba 7 wakati alipofunga mkwaju wa penalti dhidi ya Simba katika pambano la Kariakoo Derby lililoisha kwa sare ya 1-1 na tangu hapo hakufanikiwa kufunga tena, japo katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar alitoa pasi ya mwisho ya bao la pili kwa timu yake.

Achana na Sarpong, naye Nchimbi ambaye msimu huu amekosa mechi nne tu, lakini hakuna bao amefanikiwa kufunga mpaka sasa katika timu yake jambo ambalo limewashangaza mashabiki wa klabu hiyo na hata kocha wake, Cedric Kaze aliyeapa kula nao sahani moja ili warejeshe makali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaze alisema katika mazoezi yao wamekuwa wakifanya mazoezi mengi ya kufunga, lakini bado katika mechi zao hali ya kufunga imekuwa ngumu.

Kaze alisema timu yake imekuwa ikitengeneza nafasi nyingi na shida bado ipo katika kutumia nafasi hizo, hata hivyo bado hawawezi kukata tamaa na kwamba wataendelea kutumikia mbinu za ufungaj ili kuhakikisha vijana wake wenye dhima ya kuifungia timu hiyo mabao wanafanya kweli.

“Tunafanya mazoezi mengi ya kufunga hili ni tatizo ambalo naona bado tunatakiwa kuendelea kutumia mbinu zaidi za kufunga kama ambavyo tunafanya, sijajua kitu gani kinawakuta vijana wangu, lakini tunaendelea kupambana ili warudi kwenye mstari,” alisema Kaze.


SHIKHALO AMKUNA

Aidha Kaze alisema kwa kiwango ambacho kipa wake, Faruk Shikalo amekionyesha katika mechi ambazo amekuwa akimpa nafasi, benchi lake limeamua sasa kuzigawanya mechi ili yeye na Metacha Mnata wawe wanapishana.

Katika mchezo wa juzi Kaze alimuanzisha kipa huyo kutoka Kenya katika mchezo wa kwanza tangu kocha huyo atue nchini huku Mkenya huyo akionyesha kiwango bora.

“Kabla ya mechi hii ya leo (juzi) nilishajua kwamba nitampa nafasi Shikhalo amekuwa katika kiwango bora kuanzia kombe la mapinduzi na mpaka sasa nafikiri tumekubaliana kwamba sasa tutakuwa tunampa mechi zaidi katika ligi kutokana na kiwango chake,” alisema Kaze.