Mastaa Yanga: Tulieni

Mastaa Yanga: Tulieni

Muktasari:

  • MASTAA wa Yanga wametoa kauli ya matumaini kwa mashabiki na kusisitiza hatoki mtu kuanzia sasa iwe Ligi Kuu Bara au Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

MASTAA wa Yanga wametoa kauli ya matumaini kwa mashabiki na kusisitiza hatoki mtu kuanzia sasa iwe Ligi Kuu Bara au Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Pamoja na Yanga iliteleza kwa baadhi ya michezo, lakini ndio inayoongoza msimamo wa ligi ikikusanya pointi 50, ikiwa imecheza mechi 23, ilishinda 14, sare nane na ilifungwa mmoja, wakati Simba ipo nyuma kwa pointi nne katika mechi 20, ilishinda 14, sare nne na ilifungwa michezo miwili.

Kiungo wa timu hiyo, Zawadi Mauya alisema bado hawajapoteza malengo ya ubingwa, licha ya kupitia changamoto alizosema zimewaimarisha na kuwa mashujaa kuhakikisha wanamaliza mechi zilizosalia kibabe, zitakazowapa mashabiki furaha.

Alisema shujaa ni yule anayeweza kupambana na changamoto, licha ya baadhi ya mechi ambazo walidondosha pointi kwa kufungwa na Coastal Union bao 1-0, huku wakitoka sare michezo nane, jambo hilo haliwezi kuwatoa katika mstari wa upambanaji hadi dakika ya mwisho.

“Shujaa hakati tamaa, haogopi changamoto, akili na nguvu zetu ni kupigania pointi tatu kwa kila mechi, morali ipo juu kusawazisha makosa ya mechi zilizopita na ndio maana tupo kambini ili kujifua vilivyo kuweza kufikia malengo yetu kwa msimu huu na hilo ni tarajio la mashabiki wetu,” alisema Mauya.

Aliwaomba mashabiki kushikamana kwa umoja wao ili kumalizia mechi zilizosalia kwa ushindi, licha ya kukiri anajua waliumizwa na matokeo ya sare na kufungwa.

Staa wa zamani wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ mwenye rekodi ya mabao 26 aliyoiweka mwaka 1999 ambayo haijavunjwa hadi sasa, alisema Yanga ina nafasi ya ubingwa, alichoshauri ni wachezaji kuongeza umakini wa kupata pointi kwa mechi zilizo mbele yao.

“Yanga inaongoza ligi kwa pointi 50 katika mechi 23, unawezaje kusema ipo nje ya harakati za ubingwa, asili ya Jangwani ni upambanaji na uzalendo naamini hilo lipo kwa wachezaji, wasishushe silaha chini hadi nukta ya mwisho ya dakika 90 ya mechi zilizosalia,” alisema.

Alisema licha Simba kuwa nyuma kwa michezo mitatu kwa Yanga iliyocheza mechi 23 na kujikusanyia pointi 50, haoni inaweza ikawa kigezo cha Yanga kuukosa ubingwa msimu huu, kwamba soka halitabiriki.

“Hakuna anayejua atapata pointi kwa mechi ambazo hajacheza ndio maana nawashauri wachezaji waendelee kupambana hadi dakika ya mwisho ili kujenga heshima kubwa ya viwango kuwa juu,” alisema.