Mastaa Simba, Yanga presha tupu!

Monday May 03 2021
mastaa pic
By Mwandishi Wetu

ZIMEBAKI siku tano tu kabla ya Simba na Yanga kuvaana katika mchezo wao wa 106 wa Ligi ya Bara, huku presha ikianza kuwapanda mastaa wa zamani wa timu hizo ambao wameshindwa kujizuia na kuanza kutabiri kitakachotokea Kwa Mkapa wikiendi ijayo.

Simba na Yanga zitavaana Mei 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam huku timu zote zikitoka kwenye mechi zao za hatua ya 16 Bora ya Michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC), lakini zikiwa kwenye nafasi mbili za juu za msimamo, Simba ikiongoza kileleni.

Kuelekea kwenye mchezo huo wa marudiano baada ya sare ya 1-1 iliyopatikana kwenye mechi iliyopita iliyopigwa Novemba 7, mwaka jana, wadau mbalimbali hususan nyota wa zamani wa timu hizo wameshindwa kujizuia na kutabiri namna pambano litakavyokuwa gumu. Wakizungumza na Mwanaspoti, mastaa hao wa wametoa mitazamo tofauti kuelekea mchezo huo, kubwa zaidi walishindwa kutabiri wakisubiri dakika 90 nani atakuwa mbabe wa mwenzake.

mastaa pic1

Zamoyoni Mogella, aliyewahi kuzichezea kwa mafanikio timu zote, alisema kwa uzoefu alionao katika mechi hizo huwa hazina ufundi wala ubora na kwamba mara nyingi zinatawaliwa na presha na kukamiana, hivyo lolote linaweza kutoka Jumamosi.

“Pamoja na Simba kuwa kwenye ubora wa hali ya juu, ili ishinde inatakiwa kucheza kwa nidhamu, wachezaji waondoe presha kwani watakutana na Yanga ambayo inabahatisha matokeo, sasa isije ikawabahatisha kama wataingia nao wao kwa mfumo wa kukamia,” alisema mkongwe huyo.

Advertisement

Naye beki aliyewahi pia kuzichezea timu hizo, Bakari Malima alisema mechi ya watani wa jadi haitegemei ubora wa timu kutokana na asili ya ushindani uliopo baina yao, jambo kubwa analoliona ni wachezaji watakaokuwa makini na nidhamu ndio watawapa kicheko mashabiki wao.

“Angalia mechi ya mzunguko wa kwanza, Yanga ilicheza kwa uwezo wa mchezaji mmojammoja, Simba ilikuwa ipo moto, lakini mwisho wa dakika 90 ziliamua zimalize kwa sare ya bao 1-1, ndio maana nasema pamoja na Yanga kusuasua katika matokeo inaweza ikazindukia kwa Simba,” alisema.

Ivo Mapunda, kipa aliyezidakia timu hiyo na kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, alisema dabi ni tofauti na mechi nyingine kutokana na presha inavyokuwa kubwa, kitakachoamua nani ashinde ni upepo utavyovuma siku hiyo.

“Simba na Yanga wachezaji wake wanakuwa na presha kubwa, sio mechi ya nani bora na nani dhaifu, yeyote anaweza akapata matokeo, kulingana na namna ambavyo uhalisia wa timu hizo zilivyo,” alisema.

Alisema kiuhalisia Simba ipo juu hata uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, tofauti na Yanga, lakini hilo haliwezi kuzuia chochote kwenye dabi.

“Yanga hakuna muunganiko kama Simba ndio maana wanafunga kwa kubahatisha, pia maandalizi ya mechi hizo yanakuwa makubwa,” alisema.

Katika mechi 105 za awali zilizowakutanisha timu hizo katika Ligi ya Bara tangu 1965, Yanga imeshinda jumla ya mechi 37, huku Simba ikishinda 31 na michezo 37 ilimalizika kwa sare.

Mchezo wao wa duru la kwanza uliopigwa Novemba 7, Yanga ilitangulia kupata bao kwa mkwaju wa penalti kupitia Michael Sarpong kabla ya Joash Onyango kusawazisha jioni kwa kichwa, huku timu hizo zikiwa chini ya makocha Cedric Kaze na Sven Vanderbroeck waliondoka kwenye timu hizo.

Advertisement