Mastaa hawa wametibua mechi za kwanza tu ligi kuu england

 LONDON, ENGLAND. JUMAPILI iliyopita, beki wa kati wa Kibrazili, Thiago Silva alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England baada ya kujiunga na Chelsea kwa uhamisho wa bure akitokea Paris Saint-Germain.

Chelsea ilinasa huduma ya beki huyo ikiamini atakwenda kuimarisha ngome yao, lakini kilichotokea kwenye mechi yake ya kwanza tu, tena dhidi ya West Bromwich Albion alijikuta akifanya kosa lililosababisha timu yake kufungwa bao la moja kwa moja.

Akiwa moto wa safu ya ulinzi kwenye mechi hiyo ya ugenini, Silva alishuhudia timu yake ikiruhusu mabao matatu kwenye kipindi cha kwanza na kuwa na mwanzo mbaya kwenye mechi ya kwanza kwenye Ligi Kuu England.

Kilichomwokoa Silva asikumbane na lawama zaidi baada ya Chelsea kusawazisha mabao yote matatu kwenye kipindi cha pili baada ya kufunga kupitia kwa Mason Mount, Callum Hudson-Odoi na Tammy Abraham na hivyo kumfanya kocha Frank Lampard kunusurika kipigo kwenye mechi hiyo.

Silva alifanya kosa lililomruhusu Callum Robinson kufunga bao maridadi kabisa, huku ukuta wake ulionekana kuwa dhaifu kwa kuwaruhusu wapinzani kufunga mabao ya haraka.

Hata hivyo, Mbrazili huyo si mchezaji wa kwanza aliyewahi kuwa na siku mbaya katika mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England baada ya jambo kama hilo la kuchemsha kwenye mechi za kwanza. Wapo waliokosa mabao ya wazi, kukosa penati na kuonyeshwa kadi nyekundu.

Hawa hapa mastaa wengine waliokuwa na siku mbaya kazini walipozitumikia timu zao kwa mara ya kwanza kabisa.

Teddy Sheringham vs Tottenham

Presha kubwa ilikuwa kwa straika Sheringham wakati alipotinga jezi ya Manchester United kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, huku akikabiliana na timu yake ya zamani ya Tottenham. Mechi hiyo haikuwa nzuri kwake ambapo, alikosa mkwaju wa penalti aliopewa apige badala ya Eric Cantona kabla ya kupoteza nafasi nyingine muhimu ya kufunga, alipopaisha mpira juu ya goli kwenye mazingira ambayo alipaswa kusukumia mpira huo nyavuni. Kilichomwokoa Sherringham kwenye mechi hiyo ni kwamba Man United ilifunga mara mbili katika dakika za mwisho na kupata matokeo.

Joe Cole vs Arsenal

Kiungo Joe Cole alionekana kwenye kiwango bora katika mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu. Mwanzoni, Cole alikuwa kwenye kiwango bora kabla ya mambo kubadilika kufuatia kuonyeshwa kadi nyekundu kabla ya mapumziko. Jambo hilo linamfanya Joe Cole kuwa miongoni mwa wachezaji ambao hawakuwa na siku njema kabisa katika siku zao za kwanza walipocheza mechi kwenye timu zao mpya.

Koscielny vs Liverpool

Mambo ni moto. Mchezaji ambaye alimponza Joe Cole kuonyeshwa kadi nyekundu katika mechi yake ya kwanza, Laurent Koscielny kwenye mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu England baada ya kutua Arsenal. Mechi yake ya kwanza ilikuwa dhidi ya Liverpool, ambapo alionyeshwa kadi mbili za njano na hivyo kujikuta akitolewa kwa kadi nyekundu katika kipute hicho kilichofanyika Anfield. Hata hivyo, baadaye Koscielny alikuja kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho cha Arsenal na kufanywa kuwa nahodha kabla ya kuondoka kwa kulazimisha wakati aliporudi kwao Ufaransa.

Gervinho vs Newcastle

Staa Muivory Coast, Gervinho alitua Arsenal na mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle United. Kwenye mchezo huo, Gervinho akiaminika ataongoza mashambulizi na kuhakikisha timu inapata ushindi, alijikuta akionyeshwa kadi nyekundu na kutolewa kwenye mechi hiyo baada ya kuhusika kwenye vurugu zilizoanzishwa na Joey Barton. Matokeo yake kwenye mchezo huo, Gervinho alijikuta akianza vibaya ajira yake mpya huko Arsenal kutokana na kuonyeshwa kadi nyekundu.

Wayne Bridge vs Arsenal

Kwenye mchezo wake wa kwanza kwenye Ligi Kuu England akiwa na kikosi kipya, beki Mwingereza Wayne Bridge alicheza dhidi ya Arsenal. Hakika ilikuwa siku mbaya kazi kwa Bridge, ambapo alihusika kwenye mabao yote matatu iliyofunga Arsenal kwenye mechi hiyo. Aliruhusu kupigwa chenga na Theo Walcott kabla ya kumfanya Robin van Persie asiwe ameotea kwenye bao jingine. Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Bridge baada ya kusababisha penalti na kufanya awe amehusika kwenye mabao yote ya wapinzani waliofunga kwenye mechi hiyo na hivyo, kumfanya kuwa na mwanzo wa hovyo kabisa.

Danny Drinkwater vs Man City

Kuchapwa 6-1 kwenye mechi yako ya kwanza haiwezi kuwa nyakati njema kabisa kwa upande wako, lakini mbaya zaidi kwenye mechi hiyo unapohusika katika mabao mawili ya kwanza ya timu yake kufungwa. Tena hali inakuwa mbaya zaidi kama aliyehusika kufunga mabao hayo ni mchezaji mwenzako wa zamani. Kiungo Danny Drinkwater baada ya kuondoka Manchester City - mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England akiwa na timu mpya alicheza na waajiri wake wa zamani, ambapo alikuwa na siku mbaya sokoni akihusika kwenye mabao mawili waliyofungwa, ambapo Riyad Mahrez, aliyekuwa naye Leicester City akiwamo kwenye orodha ya waliofunga.

Patrice Evra vs Man City

Mechi ya kwanza ya Patrice Evra kwenye Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Manchester United ni ile ya Manchester City kwenye Manchester derby. Hakika haikuwa siku nzuri kabisa kwa beki huyo Mfaransa, ambapo kwa maneno yake mwenyewe alisema: “Wakati wa mapumziko, tukiwa nyuma kwa mabao 2-0. Ferguson aling’aka. ‘Na wewe, Patrice,’ alibwata. ‘Kwako inatosha! Kaa uwe mtazamaji sasa, kwa sababu unapaswa kujifunza sana soka la Uingereza.” Baada ya mwanzo huo mgumu, baadaye, Evra aliibuka na kuwa gwiji la klabu hiyo ya Old Trafford akibeba mataji kibao chini ya kocha Sir Alex Ferguson.

Emmanuel Frimpong vs Liverpool

Staa mwingine wa Arsenal aliyekutana na siku mbaya ya kwanza tu kwenye majukumu ya kuitumikia timu yake mpya.

Kiungo Emmanuel Frimpong mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England alikabiliana na Liverpool na mambo yalikuwa magumu baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kwenye mchezo huo, huku kadi moja wapo ni ya kumchezea rafu Jordan Henderson. Mechi za kwanza zilionekana kuwa ni tatizo ambapo, alikwenda kukumbana na wakati mgumu katika mchezo wake wa kwanza huko Barnsley mwaka 2014 wakati alipoonyeshwa kadi mbili za njano na kuishia kutolewa uwanjani kwa kadi nyekundu kwenye mechi ya kwanza.

Fernando Torres vs Liverpool

Kama ilivyokuwa kwa Sheringham, ilikuwa presha kubwa kwa straika Fernando Torres katika mechi yake ya kwanza baada ya kujiunga na Chelsea kwa ada ya uhamisho wa Pauni 50 milioni akitokea Liverpool.

Kwa kipindi hicho, ada hiyo iliweka rekodi Uingereza. Torres mechi yake ya kwanza ya ligi akiwa na jezi za The Blues ilikuwa dhidi ya timu yake ya zamani ya Liverpool na hakika yalikuwa majanga makubwa kwa El Nino, ambapo alikosa nafasi kibao za kufunga kwenye dakika za mwanzo kabla ya kudhibitiwa na beki Daniel Agger na kujikuta akitolewa kwenye dakika ya 66 tu.

Rio Ferdinand vs Leicester City

Wakati beki wa kati Rio Ferdinand ananaswa na Leeds United, ada yake ilivunja rekodi ya uhamisho Uingereza. Baada ya kutua Elland Road, mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England akiwa na miamba hiyo ilikuwa dhidi ya Leicester City na hadi mapumziko, Ferdinand alikabiliana na kelele za mashabiki ‘upotevu wa pesa tu’ kwenye mapumziko tu baada ya beki ya Leeds kuruhusu mabao matatu kwenye dakika 30 za mwanzo.

Rio alitua Leeds kwa ada ya Pauni 18 milioni na kuwa rekodi mwaka 2000 ambapo alikuwa beki ghali zaidi duniani. Baadaye aliuzwa kwa dau la rekodi tena kwenda Man United ambako alishinda mataji kibao.