Mastaa hawa mguu nje ndani Simba

Muktasari:

WAKATI mastaa tisa wa Simba wakimaliza mikataba yao, wanne kati yao wamekalia kuti kavu kwa sasa kutokana ufinyu wa namba mara kwa mara kikosini.

WAKATI mastaa tisa wa Simba wakimaliza mikataba yao, wanne kati yao wamekalia kuti kavu kwa sasa kutokana ufinyu wa namba mara kwa mara kikosini.

Habari za ndani ya Simba zinasema kwamba nyota wanaomaliza mikataba ndani ya klabu hiyo ni Jonas Mkude, Miraji Athuman ‘Sheva’, Mzamiru Yassin, Erasto Nyoni, Paschal Wawa, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Francis Kahata, Meddie Kagere na John Bocco.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa miongoni mwa nyota hao wale ambao hawakuwa na nafasi ndani ya kikosi hicho watawaruhusu kutafuta maisha kwingine, ingawa vilevile itategemea na utata wa kwamba wamefungiwa kusajili utakoma vipi.

Hata hivyo, ndani ya nyota hao wanaomaliza mikataba Simba waliokalia kuti kavu mpaka sasa ni Sheva, Kahata, Kagere na Bocco ambaye hakupata nafasi ya kucheza muda mrefu kutokana na majeraha aliyokuwa nayo ingawa habari zinasema Kocha Didier Gomes amesema apewe muda mwingine.

Mpaka sasa ni nyota wawili pekee ambao wameongeza kandarasi ya kuendelea kuitumikia Simba, Wawa msimu mmoja huku Tshabalala akiongezewa miaka mitatu, ilhali Nyoni akitarajiwa kuanza mazungumzo punde.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alikiri nyota kadhaa kumaliza mikataba na kusema jukumu la nani anabaki na yupi aondoke liko mikononi mwa Gomes.

“Kocha ndiye anawajua wachezaji wake, kwa hiyo atasema nani anamhitaji kuendelea kuwepo na nani asiwepo, sisi viongozi ni utekelezaji tu na hakuna kingine,” alisema na kusisitiza kuwa kwa sasa wapo bize na Kombe la Shirikisho, Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.