Maskauti wa Yanga noma, Nabi aagiza bonge la beki wa kati

Sunday June 20 2021
maskauti pic
By Thobias Sebastian

KOCHA wa Yanga, Nabi Mohamed amesema atatumia maskauti wakubwa na mahiri wa Afrika kuisuka Yanga mpya kwa kushirikiana na viongozi.

Nabi alisema kwamba anawajua maskauti hao na atahakikisha anawatumia vilivyo kufuta makosa yaliyojitokeza kwenye miaka ya hivikaribuni na anaamini Yanga ijayo itakuwa bora zaidi ya hii ya sasa.

Kocha huyo ameliambia Mwanaspoti, ameshawaelekeza viongozi kuhusiana na maskauti hao lakini akasisitiza kwamba wa kwanza anayemtaka kutoka kwao ni beki wa kati.

Nabi alisema mapendekezo yake ya kwanza katika ripoti yake ya usajili mpya kwa viongozi wa Yanga, anataka beki mwingine mpya wa kati.

“Katika mapendekezo yangu nimewapa viongozi mbinu ya kutafuta maskauti ambao watakuwa wanasaidiana nao katika kufanya usajili wa wachezaji waliokuwa katika viwango bora,” alisema Nabi ambaye ana uraia wa Tunisia na Ubelgiji.

“Hao maskauti ndio watafanya kazi hiyo wakishirikiana na uongozi kutokana na mapendekezo yangu, lakini naamini watafanya kazi nzuri sana,” aliongeza Nabi mwenye uzoefu na soka la Afrika.

Advertisement

Licha ya Nabi kupendekeza usajili wake wa kwanza anataka beki wa kati,Yanga kwenye msimu huu tu wamesajili mabeki wa kati watatu,Abdallah Shaibu ‘Ninja’,Bakari Mwamnyeto katika dirisha kubwa.

Kwenye dirisha dogo la usajili, walifanya usajili wa beki mwingine wa kati ambaye ni Dickson Job kutokea Mtibwa Sugar kwa mkataba wa miaka mitatu.

Kutokana na mapendekezo hayo ya Nabi, kutaka beki wa kati maana yake waliokuwepo sasa, Lamine Moro, Said Juma Makapu, Mwamnyeto,Ninja na Job mmoja wapo huenda akaonyeshwa mlango wa kutokea.

Nabi ambaye hakutaka kuingia kiundani kuhusiana na jinsi usajili wake mpya utakavyokuwa, lakini habari za ndani ambazo Mwanaspoti limehakikishiwa ni kwamba amewaambia viongozi anataka sura mpya nane.

Tayari Yanga imeshamalizana na wachezaji watatu, Djuma Shabani kutokea AS Vita, Mercey Vumbi ambaye ni kiungo Mkongo lakini dili la Lazarous Kambole wa Kaizer Chiefs limekufa baada ya mchezaji huyo kutaka mshahara ambao ukiuweka kwenye uhalisia ndani ya Simba unatosha kumlipa Clatous Chama na Cris Mugalu kwa pamoja kila mwezi.

Wachezaji wazawa ambao Mwanaspoti lina uhakika wameshamalizana na Yanga ni Dickson Ambundo wa Dodoma Jiji na David Brayson wa KMC ya Jijini Dar es Salaam.

Advertisement