Mashujaa yachukua mfungaji bora

Muktasari:

  • Mussa katika msimu huo alimaliza akiwa na mabao 14 sawa na Simon Msuva aliyekuwa anacheza kikosi cha Yanga.

Dar es Salaam. Klabu ya Mashujaa imedaka saini ya aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2016/17, Abrahman Mussa kwa jili ya kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.

Mussa katika msimu huo alimaliza akiwa na mabao 14 sawa na Simon Msuva aliyekuwa anacheza kikosi cha Yanga.

Mshambuliaji huyo msimu uliopita akiwa na Ruvu Shooting alikuwa akitumika kama beki wa pembeni, kiungo mshambuliaji au mshambuliaji wa kati na alimaliza akiwa na mabao mawili.

Chanzo kutoka ndani ya timu ya Mashujaa kililiambia Mwananchi mchezaji huyo amekamilisha usajili wa kujiunga na timu hiyo kwa miezi sita na linasubiliwa dirisha dogo tu lifunguliwe ili aweze kuanza kuitumikia timu hiyo.

“Kila kitu kimeenda vizuri na kuanzia dirisha dogo basi atakuwa na sisi kweye timu yetu kuhakikisha tunaiweka sehemu nzuri,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Mussa mwenyewe alikiri kwamba atajiunga na timu hiyo katika dirisha dogo na kuhakikisha akishirikiana na wenzake kuifanya timu hiyo iwe vizuri.

Mussa alisema akishirikiana na mshambuliaji mwenzake, Adam Adam ambaye yupo kikosini ana imani wana Kigoma watapata furaha.

“Itakuwa ni vizuri sana kwa maana Mashujaa bado haijapata matokeo mazuri lakini imani ni kubwa kwenye timu, imani yangu nitakuwa na msimu mzuri nikiwa pale.

“Sikuwa na timu Ligi Kuu, nilikuwa naendelea na majukumu yangu mengine huku nikifanya mazoezi kama kawaida.”

Kinara wa mabao hadi sasa katika timu hiyo ni Adam Adam mwenye mabao manne hadi sasa.

Mashujaa inashika nafasi ya pili kutoka chini kwenye msimamo (15) ikiwa na pointi tisa, ikicheza mechi 10, imeshinda miwili, sare tatu na kupoteza tano. Timu hiyo imefunga mabao saba na imefungwa mabao 12.