Mashabiki Yanga wawadhibiti wapinzani wao

Muktasari:

Baadhi ya mashabiki wa Simba walishatangaza kuwa watakuja kwa wingi kuishangilia Zesco ikiwa ni kulipa kisasi kwa watani wao Yanga ambao waliwashangilia UD Songo.

KATIKA hali iliyojionyesha kuwadhibiti wapinzani wao mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiwafuata wenzao wanaodhaniwa kuwa ni wa Simba na kukaa nao huku wakiwazunguka.
Katika vikundi tofauti ndani ya majukwaa ya karibu na televisheni ya ndani ya uwanja mashabiki waliovaa rangi nyekundu wamekuwa wakijikusanya kwenye vikundi vichache wakiwa wameketi katika viti.
Wakati wakiwa wametulia kundi la mashabiki wa Yanga wamekuwa wakiyafuata makundi hayo na kuyazunguka wakiimba na kushangilia huku wenzao wakiwa wametulia.
Katika zoezi hilo wapo ambao walijikuta wakivutana na kusukuma huku wale wenye nguo nyekundu baadhi yao wakilazimika kuondoka.
Mashabiki wengine wa Yanga walihama zaidi na kwenda kukaa eneo hilo ambalo limekuwa likitumiwa na mashabiki wa Simba wakiwahi kuziba eneo hilo.
Katika matukio hayo hali ya kushangaza hakuna walinzi wa uwanja wala polisi waliokwenda kudhibiti matukio hayo au kuwatenganisha katika kuweka tahadhari ya kutokea vurugu zaidi.
Hata hivyo maamuzi hayo ya mashabiki wa Yanga hayana maana kwamba uwanja umejaa ambapo eneo kubwa la uwanja bado liko tupu huku wengine wakiendelea kuingia.