Mashabiki kiduchu Kirumba

ZIKIWA zimebaki dakika chache kabla ya kuanza kwa mchezo wa Ligi Kuu kati ya Biashara United na Yanga idadi ya mashabiki bado ni ndogo.

Tofauti na jana katika mchezo wa Geita Gold dhidi ya Simba ambayo karibu nusu ya uwanja ilikuwa imeshajaa leo hali ni tofauti huku majukwaa kuu nayo yakiwa na magepu mengi hadi kufikia saa 9:40 alasiri.

Tangu asubuhi kulikuwa na mwitikio mdogo wa mashabiki waliojitokeza kukata tiketi za kuingia uwanjani hapo huku kukiwa hakuna foleni zozote za  ukataji tiketi ama kuingia uwanjani.

Mpaka muda huu sehemu kubwa ya uwanja iko tupu huku mashabiki wachache wakionekana kujikusanya zaidi katika majukwaa kuu (VIP A, B na C) na jukwaa la mzunguko lililopo eneo la kuingilia katika vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo.

Hali hiyo inatajwa kuchangiwa na ratiba ya mchezo wa jana kati ya Simba na Geita Gold, mchezo wa leo kuchezwa siku ya kazi (Jumatatu) huku mashabiki wengi wakijipanga kwa mchezo wa Jumamosi nusu fainali ya kombe la Shirikisho kati ya Yanga na Simba utakaochezwa uwanjani hapo.

Hali imekuwa tofauti ukilinganisha na mara ya mwisho vinara wa Ligi Yanga walipocheza katika uwanja huo dhidi ya Geita Gold wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 ambapo kuanzia asubuhi zilishuhudiwa foleni kubwa za kukata tiketi, kuingia uwanjani huku majukwaa yakiwa yamefurika wakati wa mchezo.

Mchezo huo utaanza saa 10:00 jioni.