Manyama aibua vita mpya Simba

UJIO wa beki wa kushoto kutoka Ruvu Shooting, Edward Manyama ndani ya Simba umeelezwa unaweza kuibua vita mpya baina yake na wachezaji anaowakuta wakicheza nafasi ya beki ya kushoto.

Manyama, anayedaiwa kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Simba msimu ujao akizipiga chenga ya mwili, Yanga na Azam zilizokuwa zikimwania anatua Msimbazi kukiwa na vita ya namba baina ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Gadiel Michael.

Awali beki huyo inadaiwa alikuwa amesaini mkataba wa awali na Azam, kabla ya Yanga nao kujitosa kutaka kumrejesha kikosini, kwani alishawahi kuichezea misimu kadhaa nyuma, lakini Mwakilishi wa Yanga alikwenda katika hoteli hiyo waliopo kikosi cha Taifa Stars akiwa na mkwanja na mkataba.

Hata hivyo beki huyo anayeishi chumba kimoja na Idd Seleman ‘Nado’ alishatoweka hotelini hapo na kwenda kumalizana na mabosi wa Simba kwa kusaini mkataba wa miaka miwili, kwa dau ambalo ni dogo kulinganisha na lile aliloahidiwa Azam na Yanga.

Hata hivyo inaelezwa ujio wa beki huyo mwenye mwili wake, unaibua vita mpya Msimbazi dhidi ya Tashabalala aliyepo kikosi cha kwanza, sambamba na Gadiel aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Yanga, lakini akikosa namba mbele ya nahodha msaidizi wake huyo.

Kwa aina ya uchezaji wake Manyama, ni wazi Tshabalala na Gadiel watapaswa kujipanga upya ili kuepuka kunyang’anywa namba na beki huyo wa zamani wa Namungo FC.

“Kila kitu kwa Manyama na Simba kimeshamalizika, kwani maslahi aliyokuwa akiyataka katika usajili wake ikiwamo mshahara na kinachosubiriwa na muda wa utambulisho tu ufike na ujio wake utaongeza ushindani kikosi kwa wanaocheza nafasi hiyo, “ alisema mmoja wa viongozi wa Simba aliyeshiriki dili hilo la Manyama.

Inaelezwa Manyama amekubali kusaini Simba kwa dau dogo kulinganisha lile la Azam na Yanga kwa sababu ya kuridhishwa na ahadi za bonasi na posho nyingine atakazopewa ndani ya timu hiyo.

“Manyama ni mchezaji halali wa Simba baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili, licha ya Yanga kuonyesha nia ya dhati kumtaka kama ilivyokuwa kwa Azam iliyokuwa ya kwanza,” kigogo huyo alisema na kuongeza;

“Awali Manyama alianza kufutwa na Azam kwa dau linaloelezwa kufikia Sh 60 milioni kabla ya Yanga nao kujitosa na kumuongezea zaidi ya fedha hizo, lakini aligoma kwenda timu zote mbili na kuitaka Simba.”

Usajili huo wa Manyama umeelezwa umetokana na mapendekezo ya kocha Didier Gomes, aliyewahi kukaririwa na Mwanaspoti kuwa, ataboresha timu yake kwa kuleta silaha mpya kulingana na upungufu wa kikosi chake.

“Sina la kuongea wakati huu kwani msimu haujamalizika ila tutaboresha timu kwa wachezaji wa nguvu kulingana na mahitaji ya timu,” alikaririwa Gomes aliyepo nyumbani kwa Ufaransa kwa mapumziko.