Manula aanza na gundu

KIPA wa Simba, Aishi Manula amerejea na gundu baada ya kuruhusu mabao matano katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga uliochezwa jioni ya leo Uwanja wa Mkapa.

Manula amekaa langoni wakati timu yake ikipoteza 5-1.

Mabao ambayo ameruhusu kipa huyo kwenye mchezo wake wa kwanza katika mashindano ni kama gundu kwake kwani hakuna kipa yeyote kati ya Ally Salim, Beno Kakolanya (msimu uliopita) wala Ayoub Lakred hawajafungwa idadi hiyo kwenye mchezo mmoja.

Manula ambaye amecheza mechi hiyo mara ya mwisho kuonekana ni alipoumia Aprili 7 mwaka huu kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (ASFC), dhidi ya Ihefu katika Uwanja wa Azam Complex hakucheza mechi yoyote ya mashindano hata pale alipoanza kuwa fiti.

Kipa huyo alipopona majeraha alicheza mechi ya kirafiki, Oktoba 14 dhidi ya Dar City na alitumia dakika 40 tu.

Baada ya hapo Manula hakuwa anaonekana katika benchi zaidi ya mazoezini hadi leo alipoanza moja kwa moja katika dabi ya watani wa jadi.

Urejeo wa Manula katika timu hiyo kwenye mechi hii ulikuwa ni wa kushtua (surprise) kwa pande zote mbili upande wa mashabiki kutokana na kutotarajia jambo hilo kutokea.