Manji: Yaani Simba imetupita! Sikubali
YUSUFU Manji
MWANDISHI WETU YUSUFU Manji amekasirika! Amewaweka kitimoto wachezaji wa Yanga kwa muda wa saa moja jijini Dar es Salaam kutaka kujua sababu ambazo zimewafanya kuiacha Simba iwapite katika Ligi Kuu Bara. Tukio hilo lilijiri jana Ijumaa kuanzia saa 4 mpaka 5 asubuhi na viongozi waliohudhuria ni Mwenyekiti Lloyd Nchunga na Katibu Mkuu, Lawrence Mwalusako na kikao kilifanyika makao makuu ya klabu hiyo, mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam ambako pia wachezaji wameweka kambi kujiandaa na mechi ya kesho Jumapili dhidi ya Toto African mjini Morogoro. Manji alitaka kujua sababu kubwa ya Yanga kuyumba na kutoka sare tatu mfululizo dhidi ya Azam, JKT Ruvu na African Lyon baada tu ya kuifunga Simba bao 1-0 jijini Mwanza Oktoba 16 mwaka huu. Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinadai kuwa Manji ambaye amekuwa hasikiki kwa kipindi kirefu sasa aliambiwa na wachezaji hao kuwa matatizo ni mawili tu yanayowakwaza ambayo ni viwanja chakavu vya mikoani na kukamiwa na timu pinzani. La ajabu kikao hicho kilifanyika bila kuwapo kwa kocha Kosta Papic ambaye alikuwa kwake maeneo ya Mikocheni. Habari hizo zinasema kuwa wachezaji walioruhusiwa kuzungumza kwa niaba ya wenzao ni Kenneth Asamoah (washambuliaji), Nurdin Bakari (mabeki) na Abdi Kassim (viungo) na wameahidi kushinda mchezo wa kesho Jumapili dhidi ya Toto African kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Mashabiki wa Yanga pamoja na viongozi wamekuwa wakikuna vichwa baada ya timu hiyo iliyoanza ligi kwa ushindi kutoa sare tatu mfululizo zilizoitoa kileleni mwa ligi na kuipa nafasi Simba ya kuongoza. Mwalusako alipoulizwa kwamba nini kilijiri zaidi mbele ya Manji alisisitiza kuwa; "Kulikuwa na kikao cha kujadili mambo ya kawaida kabisa ya ndani na mwenendo wa timu, ni siri za ndani nyie haziwahusu, zingewahusu tungewaita." Lakini inadaiwa kuwa Manji pamoja na uongozi haujardhishwa na hali ya matokeo ya sasa na unataka kuona wachezaji wakiongeza kasi zaidi. Simba inayocheza na Majimaji kesho mjini Songea inaongoza ligi kwa pointi 24 na Yanga ikifuatia kwa 22