Maneno kidogo, tukutane saiti

PAZIA la msimu wa 2023/2024, linazinduliwa rasmi leo kwa mchezo wa kwanza wa Ngao ya Jamii kati ya mabingwa watetezi Yanga dhidi ya Azam FC, katika mechi kali na ya kusisimua itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuanzia saa 1:00 usiku.
Mchezo huo ni wa kuashiria ufunguzi wa Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza rasmi Agosti 15, huku Yanga ikiwa na rekodi nzuri baada ya kutwaa mataji yote msimu uliopita kuanzia Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).
Mshindi kati ya timu hizo atakutana na mshindi kati ya Simba na Singida Fountain Gate zitakazocheza kesho katika nusu fainali ya pili kusaka tiketi ya fainali Agosti 13, kwenye Uwanja huo huo, baada ya timu zote kuficha makucha kwenye mechi zake, sasa ni muda wa kazi na kila mmoja yupo saiti kutafuta heshima, siyo kujipima tena.
MECHI YA KISASI
Azam inakutana na Yanga ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza bao 1-0 katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), iliyochezwa Julai 12, msimu uliomalizika kwenye Uwanja huohuo wa Mkwakwani Tanga.
Tangu kuanza kwa michuano ya Ngao ya Jamii mwaka 2001, timu hizo zimekutana mara nne katika fainali na Yanga imekuwa mbabe zaidi ya wapinzani wake kwani imeshinda mara tatu huku Azam FC ikishinda mara moja tu.
Licha ya utemi huo ila Yanga pia ndio inayoongoza kutwaa taji hili mara nyingi zaidi ya timu yoyote na imelitwaa mara saba (7) kuanzia mwaka (2001, 2010, 2013, 2014, 2015, 2021, 2022) na tatu kati yake imeifunga Azam.
Mwaka wa kwanza miamba hiyo kukutana ilikuwa 2013 na Yanga ilishinda bao 1-0, na 2014 zikakutana tena na Azam kuchezea kichapo cha fedheha cha 3-0 na mwaka mwingine uliofuatia wa 2015 ikacharazwa kwa penalti 8-7.
Mwaka 2016, Azam iligoma kuendeleza uteja dhidi ya Yanga ambapo iliibuka na ushindi kwa mikwaju ya penalti 4-1 na kutwaa taji lake la kwanza la michuano hiyo baada ya mchezo huo kumalizika dakika 90 kwa sare ya mabao 2-2.
VITA YA SENEGAL NA ARGENTINA
Yanga inaingia katika mchezo huu ikiwa na kocha mpya raia wa Argentina, Miguel Gamondi aliyechukua nafasi ya Nasreddine Nabi aliyeachana rasmi na kikosi hicho msimu uliopita na kutimkia klabu ya FAR Rabat ya Morocco.
Gamondi anakabiliwa na presha zaidi kutokana na mafanikio ya mtangulizi wake Nabi, ambaye aliipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kuipelea timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
Wakati Gamondi akikabiliwa na hilo pia Azam itaingia katika mchezo huo ikiwa na kocha mpya, Youssouph Dabo raia wa Senegal ambaye naye msimu huu utakuwa ni wa presha kubwa kwake kutokana na usajili uliofanyika.
Faida kubwa kwa Dabo huenda ikawa ni michezo mingi mikubwa ya kirafiki aliyocheza na timu kubwa za nchini Tunisia wakati wa maandalizi ya msimu kwa mfano Esperance na US Monastir ambazo zimekuwa ni kipimo kizuri.
KAZI IPO HAPA
Wakati kila timu ikitamba kufanya usajili wa maana ila macho yataelekezwa zaidi kwa mastaa wawili, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Yannick Bangala ambao waliachana na Yanga msimu ulioisha na kutimkia kwa matajiri Azam.
Mbali na nyota hao ila kwa upande wa Yanga mashabiki wao watakuwa wakimuangalia mshambuliaji wao mpya, Hafiz Konkoni kile atakachokifanya kutokana na kubebeshwa zigo la aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Fiston Mayele ambaye msimu uliopita alimaliza akiwa mfungaji bora.
Konkoni aliyetokea timu ya Bechem United ya Ghana anakabiliwa na mtihani wa kuziba nafasi ya Mayele aliyetua klabu ya Pryamids ya Misri ambapo msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao 17.
Mbali na hilo ila alibuka pia mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akifunga mabao saba jambo ambalo mashabiki wengi wa Yanga wanataka kuona ni kwa jinsi gani nyota huyo atawafikisha katika nchi ya ahadi msimu huu.
KAULI ZA MAKOCHA
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo Kocha Mkuu wa Azam, Youssouph Dabo anasema michezo mingi ya kirafiki aliyocheza imemsaidia kutengeneza muunganiko mzuri wa kikosi hicho huku akifurahishwa na morali iliyopo.
“Kila kitu kinaenda vizuri na sasa tuko tayari kuonyesha kile ambacho tumekifanya kwenye maandalizi yetu kwa zaidi ya wiki tatu, tunaiheshimu Yanga kwa sababu ni timu nzuri ingawa malengo ni kupata ushindi,” anasema.
Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alinukuliwa na gazeti hili akisema licha ya ugumu wa mchezo huo ila hii ndio njia sahihi kwao ya kuonyesha ni kwa jinsi gani wako tayari kutetea mataji yao waliyotwaa msimu ulioisha.