Mandonga humwambii kitu kwa Pacome Yanga

Muktasari:

  • Mandonga amesema kwamba, kabla ya Pacome, alikuwa akivutiwa zaidi na mastaa waliotimka kwenye timu hiyo, Feisal Salum 'Fei Toto' na Fiston Mayele.

Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Karim Mandonga 'Mtu Kazi', amefichua kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Yanga huku akibainisha kwamba, mchezaji ambaye huwa anapenda kumuangalia anavyocheza ni kiungo wa timu hiyo raia wa Ivory Coast, Pacome Zouzoua.

Mandonga amesema kwamba, kabla ya Pacome, alikuwa akivutiwa zaidi na mastaa waliotimka kwenye timu hiyo, Feisal Salum 'Fei Toto' na Fiston Mayele.

Bondia huyo ametoa kauli hiyo katika mahojiano maalum aliyofanya na Mwanaspoti ambapo ameeleza alivyokuwa akiwapenda mastaa hao lakini sasa Pacome ndiye mchezaji anayemkubali.

Ikumbukwe kuwa Fei Toto amejiunga na Azam msimu huu,huku Mayele akijiunga na Pyramids ya Misri baada ya kumalizika kwa msimu uliopita.

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahoajino hayo maalum, Mandonga alisema kuwa yeye katika mchezo wa soka anaipenda zaidi Yanga kuanzia kwa viongozi wake pamoja na baadhi ya wachezaji aliokuwa anawapenda licha ya kuondoka kwenye timu hiyo.

"Katika soka ukweli ninaipenda sana Yanga na viongozi wake pamoja na wachezaji ingawa wapo ambao wameondoka, lakini kila siku imekuwa ikileta matunda mapya, niliokuwa nawapenda wengine wameondoka, nilimpenda mdogo wangu Mayele, Simon Msuva, Fei Toto na mwingine ni Tuisila Kisinda.

"Mayele nilikuwa nampenda kutokana na vitu alivyokuwa anavifanya, kama katika ngumi basi ni kama Mandonga Mtu Kazi maana yeye akifunga bao lazima ateteme, ila kwa sasa habari ni Pacome japokuwa hachezi peke yake, ila moyo wangu umetokea kumpenda yeye," alisema Mandonga.