Mambo Sita Simba v Pamba Ligi Kuu Bara

Muktasari:
- Kwanza, je Simba itaendeleza mwendo wa kufunga angalau bao moja katika mechi 19 mfululizo za Ligi Kuu?
WAKATI Simba itakapokuwa mwenyeji wa Pamba Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Alhamisi hii kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, kuna mambo sita yanayopaswa kuangaliwa zaidi kutokana na takwimu zilivyo.
Kwanza, je Simba itaendeleza mwendo wa kufunga angalau bao moja katika mechi 19 mfululizo za Ligi Kuu?
Mara ya mwisho kushindwa kufunga bao ilikuwa Oktoba 19, 2024 ilipofungwa 1-0 na Yanga. Baada ya hapo imecheza mechi 18 za ligi ikifunga mfululizo.
Pili kinaihusu Pamba iliyo na mwendelezo mzuri wa kutikisa nyavu za wapinzani ikifanya hivyo katika mechi nne mfululizo, kwa Simba itakuwaje? Mara ya mwisho Pamba kushindwa kutikisa nyavu ni siku ilipolala 3-0 kwa Yanga, Februari 28 na sasa inakabiliana na Simba inayocheza mechi za viporo, ikitoka kushinda mbili dhidi ya Mashujaa na JKT Tanzania, kwa Pamba Jiji itakuwaje ikiwa kwenye harakati zake za kuifukuzia Yanga kileleni?
Pamba haipo sehemu salama katika msimamo ikitofautiana pointi tano pekee na timu iliyopo mstari wa kushuka daraja moja kwa moja, itajikwamua mbele ya Simba au itazidi kudidimizwa?
Jambo la tano, Simba ndio timu pekee iliyopoteza mechi chache zaidi uwanja wa nyumbani ambayo ni moja, mfupa huu mgumu Pamba inakabiliana nao vipi, itaweza kuitibulia Simba?
Mwisho kabisa ni Jean Charles Ahoua wa Simba, baada ya kuwa kinara wa ufungaji kwa muda mrefu akifunga 12 kisha kuzidiwa bao moja na Clement Mzize wa Yanga wakati akiwa na majukumu ya mechi za kimataifa, hii ni nafasi yake ya kurudisha ufalme wake au itakuwa tofauti?
Majibu ya hayo yote yatapatikana baada ya dakika tisini za mchezo huu wenye umuhimu mkubwa kwa timu zote mbili.
Simba inakutana na Pamba Jiji baada ya duru la kwanza kushinda 1-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kupitia bao la Leonel Ateba kwa penalti dakika ya 22 na ipo nafasi ya pili kwa sasa ikiwa na pointi 63 baada ya kucheza mechi 24 ikishinda 20, sare tatu na kupoteza moja, ikifunga mabao 55 na kufungwa tisa.
Pamba katika mechi 26 ilizocheza ipo nafasi ya 13, imekusanya pointi 27 zilizotokana na kushinda mara sita, sare tisa na kupoteza 11.
Rekodi zinaonyesha msimu huu katika Ligi, Simba ndio timu iliyopoteza mechi chache zaidi uwanja wa nyumbani ambayo ni moja ilipofungwa na Yanga, huku ikishinda tisa na sare mbili, huku safu ya ulinzi imekuwa imara pia nyumbani ikiruhusu mabao sita na ikitikisa nyavu za wapinzani mara 32, ikiwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi nyumbani, lakini ya pili kwa kufunga mabao mengi zaidi nyumbani nyuma ya Yanga yenye 33.
Pamba inapokuwa ugenini, haina matokeo mazuri kwani imeshuhudia ikipokea vichapo nane katika mechi 13, imeshinda mbili na sare tatu, ikifungwa mabao 17, yenyewe ikifunga mabao saba pekee.
Mchezo huo hautakuwa mwepesi na inatokana na namna ambavyo Simba imekuwa ikicheza mfululizo ndani ya kipindi kifupi huku kocha wa kikosi hicho, Fadlu Davids akisema analazimika kubadilisha wachezaji ili kulinda utimamu wa miili.
“Kucheza mechi nne ndani ya siku 10 sio jambo rahisi tuna siku mbili katikati ya mechi ya Pamba na KMC. Sio rahisi kuingia na kikosi kilekile nitafanya mabadiliko bila kufuata mfumo, lakini naamini tutapata matokeo mazuri,” alisema Davids.
Kocha wa Pamba Jiji, Fred Felix ‘Minziro’ anafahamu kwamba mchezo huu kwake ni mgumu, lakini amekiandaa kikosi kwa ajili ya kufanya liwezekanalo ili kupata pointi za kuiweka sehemu nzuri.
“Kila timu ninayokutana nayo inafahamu mbinu ngumu ambazo nimekuwa nazo, hivyo sitarajii mchezo mwepesi hata kidogo,” alisema.