Mambo manne, Simba, Yanga kufuzu nusu fainali

OFISA habari wa Bodi ya Ligi Kuu Bara, Karim Boimanda, ametaja mambo manne ambayo anaamini yataziwezesha Simba na Yanga kufuzu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Karim amesema Serikali, Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka nchini (TFF) na uongozi imara wa timu hizo ni miongoni mwa vitu vinavyompa matumaini Simba na Yanga, zitapita mbele ya Mamelodi Sundowns na Al Ahly kwenye robo fainali.

"Simba na Yanga zina viongozi bora ambao umekuwa ukiweka mipango na uwekezaji, hapa tunazungumzia wachezaji bora na makocha wakubwa wanaofundisha timu zetu, hii sio kwa bahati mbaya ni kwa viongozi wa hizi timu wamekuwa wakijiwekea malengo makubwa kiasi cha kuajiri hawa wachezaji ama makocha wakubwa."

"Ushirikiano ambao timu hizi mbili umekuwa ukizipata kutoka TFF na bodi ya ligi, kuna wakati watu wamekuwa wakihoji mabadiliko ya ratiba ambayo bado ya ligi imekuwa ikiyafanya lakini hiyo yote ni kuzisaidia hizi timu ili zifanye vizuri kwenye michuano ya kimataifa."

"Pia ushirikiano kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali imekuwa na nafasi kubwa sana, kwanza kutengeneza mazingira ya mpira kuchezwa kwa amani na upendo, pia kutoa ushauri kwa TFF na hamasa ambazo timu zetu imekuwa ikipata kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa Samia Suluhu Hassan."

Amesema hayo leo Machi 13, 2024 wakati akichangia mjadala wa Mwananchi Space, uliandaliwa na Mwananchi Communications Ltd, wenye mada isemayo 'Ipi nafasi ya Simba, Yanga kwenye vita ya kusaka nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.