Mambo 8 mechi ya Simba, JKT Tanzania

Muktasari:

  • Jukwaa kuu linabeba watu 200 tu waliokaa wengine mtasimama mwanzo mwisho. Uwanja mzima ni watu 4000 na tiketi za mechi ni Sh.10,000 hakuna chini ya hapo. Lakini hii ni mechi ya kwanza ya  Simba kimashindano kukanyaga kwenye Uwanja huu.

Kuna mambo nane utayashuhudia kwenye mechi ya Simba na JKT Tanzania katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni Jijini Dar es Salaam.


Ni Uwanja ulioko nje kidogo ya mji.  

Jukwaa kuu linabeba watu 200 tu waliokaa wengine mtasimama mwanzo mwisho. Uwanja mzima ni watu 4000 na tiketi za mechi ni Sh.10,000 hakuna chini ya hapo. Lakini hii ni mechi ya kwanza ya  Simba kimashindano kukanyaga kwenye Uwanja huu.


Sahau viti vya plastiki, wachezaji wote kwenye huu uwanja kule ndani vyumbani kuna masofa. Lakini Simba wenyewe watakutana na mastaa wao wanne wa zamani na mmoja wa Yanga na Mtibwa kdhaa. Ila cha mwisho ni kwamba, huku si kama Kwa Mkapa. Uwanja huku utakuwa wazi saa 6 mchana kabla ya hapo endelea kaa mbali kabisa.


Ofisa Habari wa JKT Tanzania, Masau Bwire alisema “Pichi ya uwanja ipo vizuri, tumeboresha vyumba vya kubadilishia nguo badala ya viti vya plastiki, tumeweka masofa, vipo viyoyozi hata umeme ukikatika kuna jenereta,kifupi wachezaji hawatapata shida.


“Sehemu ya jukwaa litakuwa la watu maalumu linaingiza watu 200, pia mzunguko ni takribani watu elfu nne.”


Pamoja na uwanja huo kuonekana mashabiki watasimama kwa upande wa Simba haliwasumbui, kama anavyosema Katibu wa tawi la Wekundu wa Terminal ambalo kwa sasa limehamishiwa stendi ya Magufuli, Joel Mwakitalima, kwamba popote ilipo timu yao wapo.


“Tupo tayari kuisapoti timu yetu kwenye mazingira yoyote yale, kwanza tunaenda kuishangilia na siyo kukaa kwenye viti na tunaamini mchezo huo tutashinda ,”alisema.

MASTAA WA4 SIMBA


Ndani ya kikosi cha JKT Tanzania kuna wachezaji waliowahi kuitumikia Simba, wanaoweza kugeuka mwiba kwa timu yao ya zamani, kutokana na kiwango chao cha sasa.


Wachezaji hao ni kiungo, Said Ndemla (2013-2021), winga Shiza Kichuya (2016-2018), mshambuliaji Dannya Lyanga na Hassan Dilunga(2018/19) ambaye yupo nje akiuguza majeraha.


Msimu uliopita Kichuya akiwa na Namungo alifunga mabao matano na asisti tano ni mchezaji anayetumia miguu yote miwili, ana kasi na anajua kutumia nafasi na uwezo wa kupiga mashuti ya mbali.


Wakati Lyanga akiwa na Geita alifunga mabao matatu, uzoefu wake unaweza ukawa mwiba kwa mabeki wa Simba kumkaba, kwani anatumia nguvu na akili.


Ukiachana  na waliopita Simba, wapo waliocheza  Yanga kama Matheo Antony ambaye akiwa  Mtibwa Sugar alifunga mabao matano na Maka Edward aliyepanda na timu hiyo, hadi sasa ana bao moja alilofunga dhidi ya Tabora United na ndilo lililoipa pointi tatu JKT Tanzania kwenye mchezo huo.


Kuhusiana na mchezo dhidi ya Simba, Matheo alisema: “Naona ushindani utakuwa mgumu sana. Wachezaji wao ni hatari, lakini ukizisoma mbinu zao wanafungika, nimewafunga nikiwa na KMC bao moja golini alikuwa Aishi Manula, nikiwa na Mtibwa bao moja alidaka Ally Salim, kifupi hautakuwa mchezo rahisi, ila tupo tayari kupambana.”