Malijendi: Hii dabi niyakushangaza

Muktasari:

  • Yanga itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa saa 11 jioni na dabi iliyopita iliondoka na ushindi wa mabao 5-1 yakifungwa na Kennedy Musonda dakika ya tatu, Maxi Nzengeli aliyefunga mawili dakika ya 64 na 77, Aziz KI dakika 73 na Pacome Zouzoua akifunga kwa mkwaju wa penati dakika 87.

Malijendi wa Simba na Yanga wamedai mechi ya Jumamosi hii itakuwa na mambo mengi ya kushangaza lakini watakaoenda uwanjani watainjoi soka.

Yanga itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa saa 11 jioni na dabi iliyopita iliondoka na ushindi wa mabao 5-1 yakifungwa na Kennedy Musonda dakika ya tatu, Maxi Nzengeli aliyefunga mawili dakika ya 64 na 77, Aziz KI dakika 73 na Pacome Zouzoua akifunga kwa mkwaju wa penati dakika 87.

Staa wa zamani wa Simba na Mtibwa Sugar, Mussa Hassan ‘Mgosi’ ambaye kwa sasa ni Kocha Msaidizi wa Simba Queens alisema;

“Kwanza kuanzia maandalizi yake yanakuwa tofauti na utofauti wake ni kwamba kila timu inataka kupambana na kufanya vizuri kwa ajili ya kuweka heshima kwa mashabiki zao.”

 “Naiona mechi ya maajabu kwa kuwa siku zote zinapokutana timu mbili zenye fomu tofauti haijawahi kuwa ndogo na hizi timu zisiingie kwa kuangalia matokeo ya nyuma yalikuwaje bali atakaekuwa vizuri kwa siku hiyo atachukua pointi,” alisema staa huyo wa zamani wa Mtibwa.

Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Edibily Lunyamila alisema: “Hakuna ambaye hafahamu ubora wa Yanga kwa sasa lakini hiyo sio sababu ya kwamba itamfunga Simba mabao mengi kama ilivyo mwanzo hata kama wabovu lazima itapambana kuwathibitishia watu kuwa sio kama wanavyowafikiria.”

“Bado naiona mechi ya ajabu kwa timu zote mbili na timu yeyote itakayoingia kwenye mfumo wa mwenzie basi shughuli itaishia hapo.”

Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella alisema;

“Zamani kulikuwa na hekaheka nyingi za mechi ya watani wa jadi yaani tulikuwa tunatembea na daftari mwezi mzima unajua siku fulani tunakutana na mtani wetu lakini kwa sasa mitandao imekuwa kila mtu anajua siku fulani tunacheza,

“Mechi iliyopita Simba iliingia kwa kujiamini sana kilichotokea ikafungwa mabao mengi vivyo hivyo kwa Yanga isijiamini kwa kuwa Simba mbovu huwa zinashangaza sana timu hizo zinapokutana,” alisema mkongwe huyo.