Makocha wazawa waikimbia nafasi ya Amunike

Muktasari:

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau alisema mara baada ya kutangaza nafasi hiyo makocha kutoka nchi mbalimbali Afrika na Ulaya wameomba lakini hakuna kocha mzawa aliyetuma maombi ya kuifundisha Stars.

TANGU kutimuliwa kwa aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania  'Taifa Stars' Emmanuel Amunike nafasi hiyo ipo wazi, ingawa Stars inakwenda kucheza mechi ya kufuzu fainali ya CHAN, dhidi ya Kenya keshokutwa Jumapili wakiwa na makocha wa muda chini ya Kaimu kocha mkuuEttiene Ndayiragije.
Ndayiragije ana wasaidizi wake wawili ambao ni Selemani Matola na Juma Mgunda ambao wote wanafundisha timu za Ligi Kuu Bara. Ndayiragije ni kocha wa Azam, Matola anaifundisha Polisi Tanzania na Mgunda yupo Coastal Union.
Shirikishi la Soka Tanzania (TFF), katika kuhakikisha wanapata mbadala sahihi wa Amunike wametangaza nafasi ya kazi kwa makocha ambao watataka kuifundisha Stars, lakini maombi zaidi ya 100 ya makocha waliomba wote ni makocha wa kigeni.
Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau alisema mara baada ya kutangaza nafasi hiyo makocha kutoka nchi mbalimbali Afrika na Ulaya wameomba lakini hakuna kocha mzawa aliyetuma maombi ya kuifundisha Stars.
Kidau alisema mbali na mchakato wa kumtafuta kocha mpya wa Stars, mchakato mwingine wa kumtafuta Mkurugenzi wa Ufundi unaendelea kwani nafasi hiyo ipo wazi mpaka sasa baada ya kuachana na Ammy Ninje.
"Akili ya viongozi wote wa shirikisho ni kuweka nguvu ya kutosha kupata matokeo mazuri katika mechi na Kenya ambayo tutacheza Jumapili, lakini upande mwingine tunaendelea na mchakato huu wa kutafuta kocha wa Stars na Mkurugenzi wa ufundi kwani ni watu sahihi kwa  maendeleo ya soka la Tanzania,"
"Mchakato wa kutafuta kocha wa Stars utaangalia mambo mengi mno kwani kutokuwa na kamati ambayo itachambua makocha hao zaidi ya 100, na kumpata mmoja ambaye atakuwa sahihi na mahitaji ya soka letu la Tanzania.
"Tunafikilia kuwapa nafasi zaidi makocha wazawa katika timu ya Taifa kwani hata kama wao wameshindwa kuomba pindi ambapo tutampata kocha mkuu tutaweka wasaidizi wake wazawa ili kumuelekeza mazingira ya nchi yetu, wachezaji na mambo mengine kutoka atakuwa mgeni," alisema Kidau.