Makocha Simba, Wydad watambiana

Makocha wa timu za Simba na Wydad AC ya Morocco kila mmoja kwa wakati wake ametamba kufanya vizuri katika mchezo wa kesho Jumanne.

Mechi hiyo ambayo ni ya marudiano hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.

Kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha amesema mchezo huu kwao ni muhimu na wanajiamini vya kutosha baada ya kucheza nao mchezo wa kwanza Morocco na kufungwa bao 1-0.

"Hii ni timu kubwa lakini tulishacheza nao na ulikuwa mchezo mzuri, kwa sasa wana kocha mpya na namjua ni rafiki yangu na kocha mkubwa lakini tunajiamini;

"Tunacheza mechi hii na tuna kila sababu ya kushinda mchezo huu, tutakosa wachezaji wawili eneo la kiungo lakini wengine wote waliobaki wanaweza kucheza na kuonyesha soka zuri kwa mashabiki wetu."

Upande wa Nahodha Simba, Mohamed Hussein 'Tshabalala' amesema wanafahamu umuhimu wa mchezo huu kwani kwao ni fainali na wameshasahau matokeo ya mchezo uliopita.

"Sisi kama wachezaji hatuna presha yoyote ile, tupo nafasi ya mwisho kwenye kundi letu lakini kuanzia mchezo huu tukipata matokeo basi yatafufua matumaini ya kuendelea kwetu," amesema.

Kocha mkuu wa Wydad AC, Faouzi Benzarti amesema mechi hiyo ni muhimu kwa timu zote mbili kila mmoja akitaka matokeo ya ushindi hivyo kutakuwa na dakika 90 za nguvu.

Benzarti amesema kwa asilimia 90 wapo vizuri kucheza mechi hiyo hivyo watarajie kuona soka zuri kwa timu zote mbili kwa sababu kila mchezaji wake anajua umuhimu wa mchezo huo.

"Tupo tayari kupambana ndani ya dakika 90, kila mmoja najua anataka ushindi hivyo utakuwa mchezo mgumu, lengo letu ni kushinda," amesema Benzarti.

Kipa wa Wydad, Youssef El Motie amesema jambo muhimu kwao ni kuhakikisha wanapata pointi tatu licha ya mabadiliko ya kocha hayawapi tabu.

"Sisi kwetu wachezaji wote ni profeshino hivyo hakuna tabu yoyote, tulishachukua vikombe huko nyuma hivyo hatuhofii kukutana na timu yoyote," amesema.

Simba inahitaji ushindi kwenye mchezo huo na kufikisha pointi tano huku wakiombea matokeo mabaya kati ya ASEC Mimosas dhidi ya Jwaneng.

Simba inashika nafasi ya mwisho (nne) ikiwa na pointi mbili, Wydad inashika nafasi tatu ikiwa na pointi tatu, ASEC Mimosas inashika nafasi ya kwanza ikiwa na pointi saba huku nafasi ya pili Jwaneng Galaxy ikiwa na pointi nne.